Mwanafunzi Tabora Girls adaiwa kuishi shule na ujauzito hadi kujifungua

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:02 PM Jun 11 2025
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha.
Picha:Mtandao
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo kumuandikia Barua Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera kufatilia sababu zilizowafanya Wauguzi wa Kituo cha Afya cha Biharamulo kufanya udanganyifu kwa kujaza (Medical Form) ya kuripoti kidato cha tano ambayo inaonyesha hakuwa na tatizo lolote ili hali akiwa tayari ni mjamzito.

Amesema hatua hiyo ilisababisha binti huyo kuishi na ujauzito shule kwa miezi tisa kwa madai kuwa hakutambulika mbaka alivyoenda kupata matibabu ya kichwa na kujifungua akiwa chooni.


“Lakini pia haiwezekani mtoto anakaa muda wote huo hata walezi wa shule  wasijue kwamba ana ujauzito, hata yule aliyemsindikiza haiwezekani ashindwe kujua kuwa huyu mtoto ni mjamzito…unapeleka mgonjwa anaenda chooni muda wote narudi analia kajifungua unashindwa kujua kabisa!,” alihoji Chacha.


Amesema kwa maelezo ya binti huyo, alipata ujauzito huo na dereva bodaboda wakati anatoka Biharamulo kwenda kuchukua cheti chake Karagwe baada ya kuchelewa gari na hakuwa na hela hivyo kuchukuliwa na huyo bodaboda ambaye alimlipia sehemu ya kulala kisha baadaye kurudi kulala naye.


“Nimemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, kuwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera kwa ajili ya kufatilia swala la Kijana ambaye inasemekana ndiye aliyemlaghai mwanafunzi huyo na kumpa mimba, niendelee kutoa rai kwa Wananchi wote kwamba sitakaa kufumbia macho aina hii ya matukio hasa kwa Watoto ambao bado wana ndoto za kusoma,” alisisitiza Chacha.