Mwanasayansi Jane Goodall afariki dunia akiwa na miaka 91

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:35 AM Oct 02 2025
Mwanasayansi Jane Goodall afariki dunia akiwa na miaka 91
Picha: Mtandao
Mwanasayansi Jane Goodall afariki dunia akiwa na miaka 91

Mwanasayansi mashuhuri duniani katika tafiti za tabia za wanyama, Jane Goodall, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 91, Taasisi yake imetangaza Jumatano.

Goodall amefariki akiwa nchini Marekani wakati wa ziara ya kutoa mihadhara, kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya Jane Goodall.

Kwa zaidi ya nusu karne, Goodall alijulikana kwa utafiti wake wa kina kuhusu sokwe mtu, ambapo alibadilisha mtazamo wa dunia juu ya tabia na hisia za wanyama. Tafiti zake zilithibitisha kwamba sokwe wanaonyesha hisia na tabia zenye kufanana kwa karibu na za binadamu, jambo lililovunja mipaka ya kisayansi na kijinsia.

“Ugunduzi wa Dkt. Goodall kama mtaalamu wa etholojia ulirevolushia sayansi, na alijitolea bila kuchoka kulinda na kurejesha mazingira yetu ya asili,” ilisema taarifa ya taasisi hiyo kupitia mitandao ya kijamii.

Safari ya Goodall ilianza mwaka 1960 alipowasili katika Hifadhi ya Sokwe ya Gombe Stream nchini Tanzania, kwa mwaliko wa mtaalamu maarufu wa akiolojia na anthropology, Dkt. Louis Leakey. Wakati huo akiwa na umri wa miaka 26 na bila elimu ya juu rasmi, alianzisha utafiti uliokuwa wa kipekee duniani kwa kuchunguza sokwe katika makazi yao ya asili.

Awali sokwe walimkimbia kwa hofu. “Walikuwa hawajawahi kuona nyani mweupe (mtu mzungu) kabla,” alisema Goodall katika mahojiano na Deepak Chopra mwaka 2019.

Mbali na tafiti zake, Goodall alitambulika kimataifa kwa mchango mkubwa wa kutetea uhifadhi wa mazingira. Alitunukiwa heshima ya Dame of the British Empire mwaka 2004, akapewa Tuzo ya Heshima ya Uhuru wa Rais wa Marekani (Presidential Medal of Freedom) mwaka 2025, na mwaka 2002 aliteuliwa kuwa Balozi wa Amani wa Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) ulieleza:
“Goodall alifanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya sayari yetu na viumbe wake wote, akituachia urithi wa kipekee kwa binadamu na mazingira.”

Kazi na maisha yake pia yalioneshwa kwenye filamu na vipindi vya televisheni, ikiwemo kipindi maalum cha “Miss Goodall and the World of Chimpanzees” kilichorushwa na CBS mwaka 1965 kikiwa kimenakili maisha yake Gombe, Tanzania.

Goodall ataendelea kukumbukwa kama mwanamke shujaa, mtafiti na mtetezi wa mazingira aliyeacha alama isiyofutika katika historia ya sayansi na dunia kwa ujumla.