Salum Mwalimu: Tutamaliza migogoro ya wakulima na wafugaji ndani ya siku 100

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 03:43 PM Oct 02 2025
Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu.

Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, ameahidi kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji ndani ya siku 100 endapo atachaguliwa kuingia madarakani.

Akizungumza leo katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kilosa, mkoani Morogoro, Mwalimu amesema migogoro hiyo imekuwa ikitesa wananchi kwa muda mrefu huku baadhi ya watu wakiitumia kujinufaisha binafsi.

“Hii migogoro ya ardhi ni miradi ya watu. Wanaigeuza kama chanzo cha kujipatia faida. Ndiyo maana kwenye ilani ya chama chetu tumeweka wazi kuwa ndani ya siku 100 za serikali ya CHAUMMA lazima tuimalize kabisa,” amesema Mwalimu.

Ameongeza kuwa haiwezekani changamoto hiyo iendelee kuongezeka kila siku bila suluhu ya kudumu, huku viongozi wakionekana kwenda kwa wananchi bila kuchukua hatua za kweli.

“Wakulima na wafugaji wanaoteseka ni Watanzania wenzetu. CHAUMMA tukipewa ridhaa, tutahakikisha tatizo hili linamalizika mara moja,” amesisitiza.