RIPOTI MAALUM; Utitiri vituo vya mafuta unavyoacha kitendawili

By Beatrice Moses ,, Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:27 PM Oct 02 2025
Nishati hiyo hupatikana vituo maalum vilivyosajiliwa na EWURA
Picha: Mtandao
Nishati hiyo hupatikana vituo maalum vilivyosajiliwa na EWURA

KATIKA miaka ya karibuni, Jiji la Dar es Salaam na miji mingine mikubwa nchini limekumbwa na ongezeko la haraka la vituo vya mafuta, hali inayozua maswali mengi miongoni mwa wananchi na wadau wa sekta ya mipango miji.

Kati ya maeneo yanayojengwa vituo hivyo, sehemu kubwa ni karibu kabisa na makazi ya watu, hali inayotajwa kuwa tishio kwa usalama na afya ya jamii.

Licha ya kuwapo sheria, miongozo na taratibu zinazopaswa kuzingatiwa kabla ya ujenzi, zikiwamo za kuweka umbali kati ya kituo kimoja na kingine, pamoja na kutoka kwenye makazi ya watu, utekelezaji wake bado ni changamoto.

Wachambuzi wa masuala ya usalama wa miji wanasema kasi ya ujenzi wa vituo vya mafuta haijaendana na elimu kwa wananchi juu ya tahadhari za moto na athari za kiafya zitokanazo na kuwapo vituo hivyo karibu na makazi. 

Endapo ajali itatokea, iwe ni mlipuko, moto au uvujaji kemikali, madhara yanaweza kuwa ya kutisha: vifo, majeraha, uharibifu wa mali na hata uchafuzi wa mazingira.

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula, aliwahi kutoa onyo kali kuhusu jambo hili. Akiwa bungeni alitaja umbali unaokubalika wa vituo vya mafuta kutoka mita 200 hadi 500 kutoka kwenye makazi, akisisitiza kuwa idadi kubwa ya vituo inavyoibuka kila kona ni dalili ya udhibiti hafifu.

"Leo hii unaweza kukuta vituo viwili vya mafuta vimetenganishwa kwa mita 50 au 100, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa wakazi," alisema Dk. Angelina.

SAUTI ZA WANANCHI

Wakazi wa maeneo kama Mikocheni, Tabata, Madale na Mbezi wamekuwa mstari wa mbele kulalamikia hali hiyo. 
Prof. Anna Tibaijuka, aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi, alijiunga na wakazi wenzake wa mtaa wa Ally Hassan Mwinyi ulioko

Mikocheni wilayani Kinondoni, kupinga ujenzi wa kituo cha mafuta karibu na makazi yao, akisema:

"Barabara yenyewe ni finyu ya mtaani, si mahali sahihi kwa kituo cha mafuta, kwani si tu kinahatarisha usalama, bali pia kinaweka mazingira ya kiafya kwenye hatari," alisema Prof. Anna.

Fulgence Massawe, mkazi wa Tabata, anaongeza kuwa mbali na hofu ya moto, harufu kali ya petroli inayoambatana na vituo hivyo kwa karibu inaweza kuathiri afya ya wakazi kwa muda mrefu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaonya kuwa kemikali kama benzene, toluene, na xylene zinazotoka kwenye mafuta ya petroli zina madhara kwa binadamu ikiwa ni pamoja na saratani, matatizo ya upumuaji, kizunguzungu na matatizo ya akili kwa muda mrefu.

MAZINGIRA HATARINI

Shirika la Ulinzi wa Mazingira la Marekani (EPA) linaeleza kuwa matangi ya mafuta ya chini ya ardhi yanapovuja, huchafua udongo na vyanzo vya maji. Na uchafuzi huu unaweza kudumu kwa miaka mingi. 

Kelele, msongamano wa magari na mwanga mkali wa usiku kutoka kwenye vituo hivyo pia vinatajwa kuvuruga ustawi wa maisha ya wakazi wa karibu.

Shirika hilo pia lina angalizo kuwa wingi wa vituo vya mafuta unaweza kuchangia zaidi kelele za magari na uwezekano wa viwango vya juu vya ajali karibu na maeneo ya makazi.

Linasema watu wanaoishi karibu na vituo vya mafuta, hasa watoto na wazee, pia wanaweza kukumbwa na viwango vya juu vya pumu, na hali nyingine za kupumua kutokana na uchafuzi wa hewa.

Pia linasema vituo karibu na makazi vinaweza kusababisha hofu au mfadhaiko kwa baadhi ya watu, ambao wanaweza kuwa na wasiwasi kuhusu hatari zinazoweza kusababishwa na kituo hicho ukiwamo wasiwasi wa jumla wa usalama unaoweza kuathiri ustawi wa akili.

Vilevile, Chama cha Kimataifa cha Ulinzi wa Moto (NFPA) kinabainisha kwamba, vituo vya mafuta vinahusisha vimiminika vinavyoweza kuwaka na kusababisha hatari kubwa ya moto unaoweza kuleta madhara kwa makazi ya karibu.

"Magari yanayotoka na kuingia kituoni yanaweza kusababisha ajali, ikiwa ni pamoja na kwa watembea kwa miguu au magari kugongana, hasa katika maeneo ya makazi yenye watu wengi na watoto au wazee.

"Vituo vya mafuta huhifadhi kiasi kikubwa cha mafuta, na katika tukio la kupasuka kwa tangi au kuvuja, hatari ya moto au mlipuko inaweza kuongezeka, hasa ikiwa iko karibu na nyumba," inaelezwa katika ripoti ya chama hicho.

HALI ILIVYO

Ufuatiliaji wa waandishi wa ripoti hii umebaini kuwa kwenye barabara ya Morogoro, kutoka Mbezi hadi Ubungo Mataa (umbali wa kilomita 10), kuna vituo vinane.

Huko maeneo ya Wazo, hali inatajwa na wenyeji kuwa mbaya. Kati ya Tegeta Kibaoni hadi Madale Mwisho (umbali wa Km 7), kuna vituo 11 vya mafuta. 

Katika baadhi ya maeneo kama Mbezi Mwisho hadi Segerea, Elly Msafiri anasema kuna zaidi ya vituo 13 vya mafuta na gesi. Idadi hii inazidi kuibua maswali kuhusu uthabiti wa udhibiti.

MAMLAKA ZAJITETEA 

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linasema limekuwa likihusishwa katika mchakato wa kuidhinisha ramani na kutoa ushauri wa kiusalama kabla ya ujenzi wa vituo kuanza. Mrakibu Msaidizi wa Jeshi hilo, Jamila Kindamba anasema:

"Kabla ya ujenzi, wamiliki hutakiwa kuwasilisha ramani kwa ajili ya mapitio. Tunashauri eneo lifuate taratibu zote za usalama na tahadhari za moto. Pia tunatoa mafunzo kwa wafanyakazi na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara."

Hata hivyo, Kindamba anakiri kuwa suala la 'utitiri' wa vituo vya mafuta ni mtambuka na linahusisha mamlaka nyingi kama halmashauri, manispaa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).

"Rai yetu kwa wananchi wanaokaa karibu na vituo hivi ni kutoa taarifa mapema pale wanapobaini uvunjwaji kanuni za usalama ili hatua stahiki zichukuliwe kwa haraka," anasema.

Mhandisi Ibrahim Kajugusi kutoka EWURA anasema ujenzi wa vituo karibu na wananchi unalenga kurahisisha upatikanaji huduma. Hata hivyo, anasisitiza kuwa leseni na vibali hutolewa baada ya taratibu zote kufuatwa.

Ikumbukwe kuwa Sheria ya Mafuta Na. 21 ya Mwaka 2015 inaipa mamlaka EWURA, kusimamia shughuli za sekta ya mafuta ya petroli. 

Kifungu cha 126 (1) cha sheria hiyo kinaelekeza kuwa, mtu yeyote anayetaka kujenga miundombinu ya mafuta, aombe kibali cha ujenzi EWURA.

Kwa mujibu wa muhtasari wa EWURA wa mwaka wa fedha 2023/24, vibali 300 vilitolewa kwa ajili ya miundombinu ya mafuta. Kati ya hivyo, vibali 294 vilihusu vituo vya mafuta mijini, huku 119 vikiwa vya vijijini.

Kati ya vibali vilivyotolewa, viwili vilikuwa vituo vya mafuta vya matumizi binafsi, kimoja kwa ajili ya mtambo wa kuhifadhi na kujaza gesi ya kupikia, viwili kwa ajili ya miundombinu ya kupakia na kupokea mafuta mafuta baharini," inaelezwa kwenye muktasari huo. 

WASIMAMIZI MAJENGO

Daniel Matondo, Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), anasema ujenzi wa vituo vya mafuta unapaswa kuhakikisha majengo yanakuwa imara na salama kwa matumizi ya binadamu.

"Ni majengo ya kibiashara ambayo mara nyingi yanahusisha huduma zingine kama maduka makubwa. Tunahakikisha ujenzi unaendana na viwango vinavyokubalika kitaalamu na kisheria," alisema.

Matondo, ambaye kitaaluma ni mbunifu majengo, anaongeza: "Sisi tunahusika katika kusimamia uimara wa jengo husika lakini kuna taasisi nyingine zinawajibika kwa nafasi zao, kama halmashauri ndiyo wamiliki wa viwanja wakionesha kuwa hapa panaruhusiwa kujenga kituo cha mafuta. EWURA wanatoa kibali, sisi tunafanya kazi zetu kwa kuzingatia ubora na usalama unaotakiwa," alisema Matondo.