Wanawake 81 wamehitimu mafunzo ya bure ya ufundi kupitia Chuo cha VETA Shinyanga, chini ya programu ya Wanawake na Samia. Mahafali hayo yamefanyika leo Oktoba 2, 2025, yakihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mhita amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha programu hiyo inayowawezesha wanawake kupata ujuzi wa ufundi na kujikwamua kiuchumi.
“Mafunzo haya yamewajengea uwezo wa kujiajiri na kuimarisha uchumi wa familia zao,” amesema Mhita.
Aidha, amewataka wahitimu kuunda vikundi vya ujasiriamali ili wapate mikopo ya Halmashauri isiyo na riba, ambapo wanawake hunufaika kwa asilimia 4 ya mikopo hiyo, sambamba na kuchangamkia fursa za taasisi nyingine za kifedha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Samia Taifa, Futuma Madidi, amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia wanawake nafasi ya kujifunza ufundi, huku akiiomba serikali kuwapa wahitimu hao kipaumbele kwenye zabuni na fursa nyingine za kiuchumi.
Naye Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga, Abraham Mbughuni, amebainisha fani walizosoma wahitimu na idadi yao kuwa ni saluni (25), mapambo (4), umeme (10), kompyuta (2), bomba (7), udereva (4), ushonaji (26) na mapishi (3).
Baadhi ya wahitimu akiwemo Zainabu Joseph, wameishukuru serikali kwa kuwapatia fursa hiyo, wakisema imewajengea ujuzi wa kuendesha maisha na kujipatia kipato.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED