UCHAGUZI MKUU: Kanisa Katoliki latoa msimamo

By Restuta James , Nipashe
Published at 12:10 PM Oct 02 2025
Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Yuda Thaddeaus Ruwa’ichi.

Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam limetoa msimamo wake rasmi likisisitiza kuwa halina mgogoro wala mvutano wowote na serikali, na kuwataka waamini wake kuwa makini na taarifa za upotoshaji zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Yuda Thaddeaus Ruwa’ichi, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilee ya miaka 25 na 50 ya upadre, kwa baadhi ya mapadre wa jimbo, iliyofanyika katika Parokia ya Msimbazi Center, jijini Dar es Salaam.

Katika mahubiri yake, Askofu Ruwa’ichi alieleza kusikitishwa na kusambaa kwa taarifa za uongo mitandaoni, hususan tangazo linalodaiwa kuwa la semina kwa waamini litakalofanyika Oktoba 29, 2025, akieleza kuwa tangazo hilo si sahihi na halijatolewa na ofisi ya jimbo.

"Wale mnaopita mitandaoni, mmeona tangazo la semina ya walei tarehe 29 Oktoba. Ninaomba niweke wazi, halijatoka katika ofisi yangu, halina sahihi yangu wala ya Katibu Mkuu. Si tangazo rasmi," alisema Askofu Ruwa’ichi.

Alibainisha kuwa tarehe sahihi ya tukio hilo kwenye kalenda ya kanisa ni Novemba 29, 2025, na kuonya kuwa upotoshaji huo unalenga kuchochea hisia za kimakundi na kuwasilisha picha isiyo sahihi ya uhusiano kati ya kanisa na serikali.

"Sisi kama Kanisa Katoliki hatuna mpango wa kushindana, kulumbana wala kushikana mieleka na serikali. Wote wenye mawazo kama hayo, wajue kwamba hawatoki kanisani, bali kwenye mitandao yenye nia mbaya," alisisitiza.

"MUWE MACHO"

Askofu Ruwa’ichi aliwaasa waamini kuwa na uchambuzi wa kina wanaposoma au kusikia taarifa mtandaoni, na kutoruhusu mihemko kuwaongoza katika uamuzi au hisia zisizo sahihi.

"Mnapoona tangazo limewekwa mtandaoni, msianze kuhaha... litazameni kwa macho ya kiroho, lihojini, mlinganishe na taarifa rasmi za kanisa. Tusifanye uamuzi kwa misukumo ya nje," aliongeza.

Katika sehemu nyingine ya mahubiri, Askofu Ruwa’ichi aliwataka mapadre wote kuendelea kuwa nguzo ya utakatifu, uadilifu na upendo, kwa kuwa wito wao umetokana na neema ya Mungu, si kwa uwezo wao binafsi.

"Ewe padre, usione fahari kuishi kwenye tope la dhambi. Hukuzawadiwa wito huu kwa ujanja wako, bali kwa huruma ya Mungu. Weka upya azma yako ya kumtumikia Mungu kwa bidii, furaha na utayari," alisema.

Aliwahimiza mapadre kuishi sifa za Kristo: kuwa walimu, viongozi, makuhani na watendaji, wakichukua nafasi zao kama mifano hai ya huduma ya kiroho kwa watu wa Mungu.

"Kumfuata Kristo si jambo rahisi – ni safari nzito inayohitaji moyo wa kujitoa na unyenyekevu wa kweli. Mapadre ni mashuhuda wa upendo, si watawala wa imani za watu, bali wasaidizi wa furaha ya kiroho ya waamini," alihitimisha.