Wadau wa afya washauri mpango bima ya afya kwa wote ufanikishwe

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 07:27 PM Oct 02 2025
Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya PharmAcces, Dk. Heri Marwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya PharmAcces, Dk. Heri Marwa.

Wadau wa sekta ya afya wameishauri serikali kufanikisha mpango wa bima ya afya kwa wote, wakisisitiza kuwa suala hilo halihitaji nchi iwe tajiri bali utashi wa kisiasa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wadau wa afya, Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya PharmAcces, Dk. Heri Marwa, amesema makundi maalumu kama watoto, wazee na wajawazito yanapaswa kupewa kipaumbele ili kupata huduma bora za afya.

“Kuna haja ya kuhakikisha kila mtu anakuwa na bima ya afya. Ili kufanikisha hilo, serikali inapaswa kushirikiana na sekta binafsi na kutumia teknolojia kufikia wananchi wote,” amesema Dk. Marwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taarifa na Mtafiti Mkuu NIMR, Mary Mayige, amesema utafiti walioufanya kwa kushirikiana na PharmAcces kuhusu Bima ya Afya kwa Jamii Iliyoboreshwa (CHF) ulibaini bima hiyo ilifanikiwa kusajili wanachama wengi kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa bima ya afya kwa wote, ambapo idadi ya waliosajiliwa ilianza kupungua.

Amesema mapendekezo yao kwa serikali ni kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinaelekezwa pia katika kuzuia magonjwa, badala ya kutumika zaidi kwenye matibabu pekee.

“Upatikanaji wa bima ya afya kwa wote unawezekana kabisa, kinachohitajika ni mikakati sahihi na dhamira ya kisiasa,” amesema Mayige.