Mdhibiti Ubora Mkuu wa Shule wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Lilian Kazenga, amewataka wadau wa elimu, sekta binafsi, asasi zisizo za kiserikali na jamii kwa ujumla kuunga mkono juhudi za kukuza utamaduni wa usomaji, hususan wa kidijitali, ili kuhakikisha watoto wanakuwa na uwezo wa kusoma na kuelewa kwa ufanisi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Usomaji yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Kilamba, Kazenga amesema jamii inapaswa kushirikiana na walimu na wadau wa elimu katika kuwahamasisha watoto kusoma vitabu vya kawaida na vya kidijitali kila siku, sambamba na kuhakikisha mazingira ya shule na nyumbani yanawajengea motisha ya kusoma.
“Ninyi ni chachu ya mabadiliko na moyo wa mfumo wetu wa elimu. Bila juhudi zenu hakuna maendeleo ya kweli yanayoweza kupatikana. Leo hii mwalimu si wa kufundisha tu, bali pia ana jukumu la kuwaongoza wanafunzi kutumia teknolojia kwa njia sahihi ili kujifunza kwa ufanisi na kwa usalama. Ninyi ndio wawezeshaji wa kizazi cha kidijitali,” amesema Kazenga.
Ameongeza kuwa serikali inaendelea kuboresha elimu kupitia maboresho ya mitaala na kuhamasisha matumizi ya TEHAMA, huku akipongeza juhudi za wadau mbalimbali katika kupunguza tatizo la kutokujua kusoma na kuandika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi wa Room to Read Tanzania, Joan Minja, amesema shirika hilo limeanza kazi nchini tangu mwaka 2012 katika Halmashauri ya Mvomero na baadaye kupanua wigo wake katika wilaya na manispaa mbalimbali ikiwemo Bagamoyo, Chalinze, Kibaha, Mkuranga, Handeni, Muheza, Korogwe, Tanga Jiji, Ubungo na Temeke.
Minja amesema kupitia Mradi wa Usomaji na Maktaba, shirika linaamini maktaba ni sehemu muhimu ya kujenga stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) na kuimarisha tabia ya kusoma miongoni mwa watoto.
“Mpaka sasa tumesambaza vitabu vya hadithi za watoto 1,474,764 vilivyoandikwa na waandishi wa Kitanzania na kuthibitishwa na Taasisi ya Elimu Tanzania,” amesema Minja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED