PSSSF yasajili askari polisi wapya 4,800

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:28 PM Jun 18 2025
PSSSF yasajili askari polisi wapya 4,800
Picha: Mpigapicha Wetu
PSSSF yasajili askari polisi wapya 4,800

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umesajili askari polisi watarajiwa 4,800 wanaokaribia kumaliza mafunzo yao katika Shule ya Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kabla ya zoezi la usajili, maafisa wa PSSSF wakiongozwa na Meneja wa Kanda ya Kati Dodoma, Michael Bujiba walitoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa askari hao wapya.

Akizungumza katika zoezi hilo kwa niaba ya PSSSF, Bujiba alisema, zoezi hilo la usajili ni ishara tosha kwamba Mfuko utakuwa pamoja nao katika maisha yao ya utumishi na maisha ya kustaafu. 

"Leo mnaajiriwa na Serikali mkiwa na nguvu zenu na mtalipwa mshahara, lakini Serikali kwasababu inawajali inawaandalia maisha yenu ya baada ya utumishi kupitia Mafao ya uzeeni," alisema Bujiba. 

Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) wa Jeshi la Polisi Makao Makuu Kitengo cha Fidia na Mafao, Basil Pandisha, ameipongeza PSSSF kwa utoaji elimu ya Hifadhi ya Jamii kwa askari hao wapya, lakini pia hata kwa askari ambao tayari wamesajiliwa.

" Elimu ya mara kwa mara inayotolewa na Mfuko imesaidia sana, changamoto chache zilizobaki na kwa wale ambao hawana tabia ya kufuatilia vizuri michango yao, hata hao tukibaini tunashirikiana na Mfuko na kutatua changamoto hizo mara moja.” Alisema SACP, Pandisha.

Aliwakumbusha kutambua kuwa wameingia kwenye ajira, lakini utafika wakati wa kustaafu hivyo ni vema wakajipanga kuanzia sasa.