RC Kunenge aipa kongole Halmashauri ya Mkuranga kupata hati safi

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 05:24 PM Jun 18 2025
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kwa kupata hati safi kwa zaidi ya miaka tisa mfululizo, huku akisisitiza kuwa mafanikio hayo yaonekane kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kunenge alitoa pongezi hizo jana Juni 17, 2025, wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza Maalum la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, kilichokuwa kikijadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Amesema upatikanaji wa hati safi unapaswa kwenda sambamba na ukusanyaji na matumizi bora ya mapato ya Halmashauri, huku akisisitiza kuwa miradi inayotekelezwa lazima iwanufaishe wananchi kwa kutatua kero zao.

Aidha, amewataka madiwani kuwasilisha mapendekezo ya miradi wanayotaka itekelezwe katika maeneo yao ili kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi na kuharakisha maendeleo.

Kwa upande wake, Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo, Cornery Sima, amesema Halmashauri ya Mkuranga imefanikiwa kupata hati safi kwa miaka tisa mfululizo. Alibainisha kuwa katika kipindi hicho, kulikuwa na hoja 33, ambapo 16 kati yake zimefungwa na saba zinaendelea kushughulikiwa.

Naye Katibu Tawala wa Halmashauri hiyo, Omary Mwanga, alisisitiza kuwa hoja zote zilizobaki zitaendelea kufanyiwa kazi kwa wakati ili kuhakikisha hazirudiwi kwenye ukaguzi unaofuata.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Mohamed Mwera, alitoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano anaoutoa kwa Halmashauri hiyo, ikiwemo ushauri na maelekezo yanayochochea maendeleo kwa wananchi wa Mkuranga.