Sheikh Ponda: ACT Wazalendo itaongoza mapambano ya kulinda kura Oktoba

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 09:13 PM Jun 18 2025
Kada mpya wa Chama Cha ACT Wazalendo, Sheikh Ponda Issa Ponda
Picha: Mpigapicha Wetu
Kada mpya wa Chama Cha ACT Wazalendo, Sheikh Ponda Issa Ponda

Kada wa Chama Cha ACT Wazalendo, Sheikh Ponda Issa Ponda, amesema katika uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, chama hicho kitaongoza mapambano ya kulinda kura za wananchi.

Amesema ni muhimu kupambana ndani ya eneo la vita kuliko nje ya uwanja wa mapambano, na kwamba hiyo ndiyo njia pekee ya kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Sheikh Ponda aliyasema hayo leo Juni 18, 2025 jijini Dar es Salaam, katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho katika eneo la Manzese.

Ponda ambaye anafahamika kwa misimamo yake ya kupigania haki za binadamu, amesema inawezekana kushinda uchaguzi ujao kwa kutumia nguvu ya wananchi kama ilivyokuwa mwaka 2010 ambapo wapinzani wengi walishinda kwa kutumia nguvu hiyo hiyo ya umma.

"Wale Polisi ni binadamu kama tulivyo sisi, inakuwaje ifike mahala ushindwe kuelewana naye? Ni binadamu mwenzako, tutatumia lugha zinazoweza kueleweka, kila mahala kuna lugha yake," amesema Ponda huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.

Amesema kwa kufanya hivyo wataweza kujenga ujasiri kwa wananchi kupambana na kutetea haki zao.

Ponda amesema hakuna sababu ya kuendelea kuwa na utawala ambao unatoza gharama kubwa kwa wafu, huku akitolea mfano wagonjwa wa figo ambao wanalazimika kutumia Shilingi 540,000 kila wiki kwa ajili ya matibabu, na endapo hawatapata fedha hizo wanakabiliwa na kifo.

"Hakuna serikali kama mtu anaweza kuchukuliwa akauawa, na waliofanya kitendo hicho wasijulikane. Tuna sababu gani ya kuendelea kuwa na serikali ya namna hii?" amehoji Ponda.

Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba, na kwamba iwapo Polisi atataka kumzuia mtu asipige kura, mtu huyo anapaswa kujua kuwa analinda haki yake ya kikatiba.

Amesisitiza kuwa mbegu ya mapambano ya kudai demokrasia lazima ianze Dar es Salaam kwa kuwa ndicho kitovu cha mageuzi yote nchini.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, alisema serikali iliyopo madarakani inatumia nguvu ya kijeshi kuendelea kubaki madarakani.

"Leo nchi yetu mauaji yamekuwa jambo la kawaida, utekaji umekuwa jambo la kawaida. Nchi inawatu wasiojulikana wanaweza kumchukua mtu kwenye gari na kesho akakutwa amekufa, na serikali inasema ni watu wasiojulikana.

"Nchi inapoteza raia wake, kwamba eti kuna watu wasiojulikana wananguvu kuliko Jeshi la Polisi. Katikati ya hali hii mnufaika mkuu ni CCM ambayo mpaka sasa haijatoa maelezo ya kina kwa wananchi kuhusu matukio hayo," amesema Mchinjita.

Ameongeza kuwa licha ya uhaba wa walimu nchini, vijana wengi waliosomea taaluma ya ualimu kwa gharama kubwa bado wapo mtaani bila ajira, huku serikali ikihitaji zaidi ya walimu 200,000 kufidia upungufu uliopo.