Wake wa Marais Afrika, Asia waungana kupinga unyanyapaa kwa wagumba

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 07:45 PM Jun 18 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Merck Foundation, Dk. Rasha Kelej.
Picha: Vitus Audax
Mkurugenzi Mtendaji wa Merck Foundation, Dk. Rasha Kelej.

Wake wa Marais kutoka nchi za Bara la Afrika na Asia wameendelea kuweka msimamo wa pamoja kuhakikisha kunakuwepo usawa wa kijinsia, elimu na afya bora sambamba na kukabiliana na unyanyapaa kwa wagumba.

Wametoa kauli hizo kwa nyakati tofauti katika Mkutano wa Saba wa Wake wa Marais, yaani Merck Foundation First Ladies Initiative (MFFLI) Summit, uliofanyika katika Umoja wa Falme za Kiarabu, jijini Dubai.

Pamoja na mambo mengine, wake hao wameeleza kuwa uwezeshaji kwa mtoto wa kike, hususan katika nchi za Afrika na Asia, ndiyo njia pekee inayoweza kumnusuru dhidi ya ndoa za utotoni pamoja na aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia.

Mke wa Rais wa Angola, Ana Lourenço, amesema watoto wa kike kuendelea kubaguliwa na kutokuwezeshwa katika nyanja za elimu, afya na uchumi ndiyo sababu kubwa ya kushamiri kwa ndoa za utotoni, unyanyasaji wa kijinsia na kushindwa kufikia ndoto zao.

Naye Mke wa Rais wa Maldives kusini mwa Asia, Sajidha Mohamed, amesema kuendelea kuimarisha huduma za afya vijijini na maeneo yasiyofikika ni njia muhimu ya kumsaidia mama na mtoto.

Kuhusu kampeni ya kupinga unyanyapaa dhidi ya ugumba, Sajidha ameshauri elimu iendelee kutolewa kwa jamii ili kuondokana na mila potofu kuhusiana na hali hiyo.

1
Awali akifungua mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Merck Foundation, Dk. Rasha Kelej, amesema kuwa sambamba na kusherehekea miaka 13 ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo, tayari wametoa ufadhili wa masomo ya nje kwa zaidi ya madaktari 2,520 kutoka nchi 52 Afrika na Asia Kusini katika nyanja 44 maalum za matibabu.

Kuhusu program ya elimu kwa mtoto wa kike, Dk. Kelej amesema tayari wamefadhili zaidi ya wasichana 1,000 walio katika mazingira magumu kutoka nchi 17, lengo likiwa ni kuwaendeleza kielimu hadi watakapomaliza masomo yao.

“Ahadi yetu ni kuendelea kufundisha wataalam wa matibabu wenye ujuzi, kusaidia elimu ya wasichana, kukomesha unyanyapaa kuhusu utasa, na kujenga uwezo katika maeneo ambayo hayajafikiwa zaidi,” amesema Dk. Kelej.

Mkutano huo ambao ni miongoni mwa makongamano yanayoendelea kwa siku mbili Dubai, unahusisha pia mafunzo kwa waandishi wa habari kupata ujuzi wa kuripoti kwa usahihi masuala ya matibabu na kuandaa habari za kijamii zinazohusu ndoa za utotoni, kisukari, afya ya akili na utasa.

Watanzania ni miongoni mwa washiriki wa mkutano huo, wakiwemo madaktari pamoja na mwandishi mmoja kutoka Kampuni ya The Guardian Ltd.