EWURA yazitaka taasisi kuweka mikataba ya huduma mtandaoni

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 05:57 PM Jun 18 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Dk. James Andilile.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Dk. James Andilile.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Dk. James Andilile, amesema taasisi zote zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo za huduma za maji, umeme, gesi asilia na mafuta, zinatakiwa kuweka mikataba ya huduma kwa wateja kwenye tovuti zao rasmi ili kuongeza uwazi, ufuatiliaji na uwajibikaji.

Dk. Andilile akizungumza kwenye maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, amesema “Wananchi wanapaswa kujua haki na wajibu wao kuhusu huduma wanazopata. Taarifa hizi lazima ziwe wazi kwa umma.” 

Aidha, amesema katika kuhakikisha huduma zinapatikana kwa ufanisi zaidi, EWURA imehamishia huduma zake mtandaoni  kuanzia leseni, usajili wa watoa huduma hadi kupokea na kushughulikia malalamiko.

"EWURA inawekeza katika Big Data na AI ili kuongeza uwezo wa kutoa huduma kwa haraka, kwa kutumia mifumo ya tahadhari ya mapema dhidi ya changamoto kwenye sekta ya nishati na maji,"amesema.