Jukwaa la nne ushirikishwaji watanzania Sekta ya Madini lilete mabadiliko – Ollal

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:45 PM Jun 18 2025
Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Madini, Augustine Ollal.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Madini, Augustine Ollal.

Wadau wa madini nchini wametakiwa kutumia Jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta la Madini kama kichocheo cha mabadiliko katika Sekta ya Madini hasa kwenye eneo la ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini katika eneo la ajira na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini kama vile usambazaji wa vifaa na vyakula.

Hayo yamesemwa jijini Mwanza leo Juni 18, 2025 na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Madini, Augustine Ollal kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo wakati akifunga Jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta la Madini.

Jukwaa hilo lililoanza mapema Juni 16, 2025 limekutanisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na  Wizara ya Madini na Taasisi zake, Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi, Taasisi za Fedha, Kampuni za Uchimbaji wa Madini na Watoa Huduma kwenye Migodi ya Madini.

Amesema kufanyika kwa jukwaa hilo ni mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Madini kuhamasisha ushiriki wa watanzania katika shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini na usambazaji wa bidhaa na huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ili wananchi waendelee kunufaika na rasilimali madini na kukuza uchumi wa nchi.

Katika hatua nyingine, amezitaka kampuni za madini kuendelea kutoa kipaumbele kwa watanzania kwenye  ajira na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.

Wakati huo huo amempongeza Waziri wa Madini Anthony Mavunde kwa kutafsiri maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hali iliyopelekea mchango wake katika Pato la Taifa kufikia asilimia 10.1.

 Jukwaa hilo lenye kaulimbiu inayosema Ongezeko la Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ni chachu ya Ukuaji wa Uchumi limeambatana na maonesho yenye lengo la kuelimisha kuhusu fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini.