Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wazabuni kuhusu matumizi ya Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo (NeST).
Akifungua mafunzo ya siku moja leo Juni 18, 2025 kwa wazabuni wa Mkoa wa Dodoma na mikoa Jirani, Jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando amewaasa kujifunza matumizi ya moduli hiyo ili waweze kuitumia wakati wa kuwasilisha malalamiko na rufaa zitokanazo na michakato ya zabuni.
Sando amesema kuwa moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST inafaida kwa wazabuni, taasisi nunuzi na PPAA ikiwemo kuokoa muda, gharama na kuongeza uwazi na uwajibikaji. “Moduli hii ina okoa muda na gharama kwa mzabuni kwa kuwa hatalazimika kusafiri ili aweze kuwasilisha malalamiko au rufaa yake PPAA,” alisema Sando
Pamoja na mambo mengine, Sando amesema PPAA imeweza kushughulikia mashauri 177 yaliyotokana na michakato mbalimbali ya Ununuzi wa Umma, ambapo katika mashauri hayo, PPAA ilizuia utoaji tuzo kwa zabuni 37 kwa wazabuni wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika, kwa kufanya hivyo PPAA iliisadia Serikali kupata thamani halisi ya fedha katika miradi hiyo.
Kwa upande wa wazabuni walioshiriki mafunzo hayo wakiongozwa na Mhandisi Beda Labule, amesema kuwa utaratibu wa kuwasilisha rufaa kieletroniki umerahisisha zoezi la kuwasilisha malalamiko na kukata rufaa kwa wazabuni ambao hawataridhika na sababu za kuondolewa kwao ikilinganishwa na ilivyokuwa awali.
“Kama mtakumbuka awali mzabuni mwenye malalamiko au rufaa alipaswa kusafiri kwenda katika Ofisi za PPAA kuwasilisha rufaa yake, ila sasa baada ya Serikali kuweka Moduli hii ya kupokea na kushughulikia malalamiko imeturahisisha zoezi la kuwasilisha malalamiko yetu PPAA,” amesema Mhandisi Labule
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Jofenai Investment, Jofenai-joy Felician amesema moduli imerahisisha zoezi la uwasilishaji wa malalamiko yatokanayo na michakato ya ununuzi wa umma pamoja na kusaidia kuokoa gharama na muda pamoja na kuongeza uwazi.
“Mimi kama mzabuni nimewahi kupatwa na changamoto mbalimbali wakati wa uwasilishaji wa rufaa kwa wakati, ni imani yangu kupitia moduli hii itasaidia pia utunzaji wa kumbukumbu za taarifa za rufaa ambazo zitakuwa zinawasilishwa katika michakato yote ya ununuzi wa umma,” amesema Felician
Mafunzo hayo ya siku moja kwa wazabuni wa Mkoa wa Dodoma na mikoa Jirani yanafuatia mafunzo ya awamu ya kwanza yaliyofanyika Kanda ya Ziwa tarehe 4 – 6 Februari, 2025 yalijumuisha mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Kagera, Simiyu na Shinyanga.
Aidha, awamu ya pili ya mafunzo yalifanyika Kanda ya Kaskazini tarehe 10 Aprili, 2025 yakijumuisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Kadhalika, mafunzo ya awamu ya Tatu yalifanyika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini tarehe 29 na 30, 2025 ambapo yalijumuisha mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED