Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umepanga kushirikiana na Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha taasisi zote za umma zinazohudumia watu zaidi ya 100, ikiwamo shule na hospitali, zinapatiwa majiko ya kupikia yanayotumia nishati safi.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Utawala wa REA, Renatus Msangira, wakati wa Maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma kuanzia Juni 16 hadi 23, 2025.
Msangira amesema tayari REA imeanza utekelezaji wa mpango huo kwa taasisi za Magereza, ambapo majiko ya nishati safi yamekwishapelekwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi hizo.
“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuhakikisha Watanzania wote wanapata nishati safi ya kupikia. Pia tunawashukuru Wizara husika, Wizara ya Fedha na wadau wa maendeleo kwa kutuwezesha kutekeleza dira hiyo,” amesema Msangira.
Kuhusu huduma ya umeme vijijini, amesema hadi sasa vijiji vyote vimefikishiwa umeme na kwamba juhudi zinazofuata ni kuhakikisha huduma hiyo inawafikia pia wananchi wa vitongoji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED