Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, ameipongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa ubunifu na ujenzi wa majengo yenye viwango vya juu vya ubora.
Akizungumza alipotembelea banda la TBA katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kwenye viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma, Waziri Simbachawene alisema:
“TBA mnafanya kazi nzuri katika ujenzi wa majengo ya Serikali. Hata jengo la Wizara ya Utumishi mmejenga ninyi, ni jengo zuri na linavutia. Hongereni sana.”
Aidha, amezihimiza taasisi za Serikali, ikiwemo TBA, kuendelea kutekeleza miradi ya umma kwa weledi na ufanisi ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
TBA ni miongoni mwa taasisi za umma zinazoshiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu, yenye kaulimbiu “Himiza matumizi ya mifumo ya kidijiti ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji.”
Katika banda la TBA, wananchi wanapata fursa ya kujifunza kuhusu miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na wakala huo pamoja na mchango wake katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.
Maonesho hayo yalianza Jumatatu wiki hii na yanatarajiwa kufungwa Juni 23, 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED