Ridhiwani aitaka ATE kuweka mkazo utendaji bora uzingatiaji Sheria za kazi

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 08:19 PM Jun 18 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,Ridhiwani Kikwete.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,Ridhiwani Kikwete.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,Ridhiwani Kikwete, ametoa wito kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kuhakikisha kinakuwa na utendaji bora utakaochochea ushirikiano madhubuti kati ya Serikali na waajiri nchini.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa ATE uliofanyika leo Juni 18, 2025 jijini Dar es Salaam, Waziri Ridhiwani amesisitiza umuhimu wa ATE kusimamia kwa umakini masuala ya wanachama wake kwa kuhakikisha waajiri wote wanazingatia kikamilifu Sheria za Kazi, hasa katika kuwapatia wafanyakazi mikataba halali ya kazi na kuandaa mazingira bora ya kufanyia kazi ili kuongeza ustawi na tija kazini.

Amesema uzingatiaji wa Sheria za Kazi ni msingi wa kulinda haki za wafanyakazi na kuwawezesha kutoa nguvu kazi yao kwa ufanisi, hali itakayowanufaisha wafanyakazi na waajiri kwa pamoja.

Aidha, Waziri Ridhiwani amewataka waajiri kuhakikisha wanalinda nguvu kazi kwa kuzingatia na kutekeleza kikamilifu miongozo ya afya na usalama kazini.

Vilevile, ametoa wito kwa waajiri wote nchini kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kisheria kwa kuwasilisha kwa wakati michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo NSSF kwa sekta binafsi na PSSSF kwa sekta ya umma, pamoja na kuchangia katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

“Kwa kufanya hivyo, mnaimarisha ustawi wa wafanyakazi, kuchochea uaminifu kazini na kujenga msingi wa ajira zenye staha na uchumi jumuishi unaozingatia utu, usawa na maendeleo ya pamoja,” amesema Waziri Ridhiwani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,Ridhiwani Kikwete.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na ATE kuboresha mazingira ya kazi, sambamba na kudumisha ushirikiano wa UTATU kwa manufaa ya sasa na ya baadaye.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba, alisema kuwa mabadiliko ya sheria ni muhimu ili kwenda sambamba na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.

“Leo tunajadili Mabadiliko ya Sheria za Kazi 2025 kwa mtazamo wa tija na uzalishaji, tukizingatia mfumo wa Utatu ili kuhakikisha usawa wa pande zote. Tija siyo juhudi pekee bali ni mkakati, kupitia sera, sheria, na maboresho ya mifumo ya kazi tunaweza kuinua uchumi na kuongeza ajira. ATE inaendelea kushauri Serikali kuhusu kupunguza tozo ya Maendeleo ya Ujuzi (SDL) hadi 2% kwani sekta nyingi zenye ajira nyingi zinaathiriwa moja kwa moja na gharama hii. Tumefanya mchakato wa mabadiliko ya sheria kuwa wazi ili kila mwajiri aelewe kwamba ATE ilikuwa mstari wa mbele, uwajibikaji na uwazi ni misingi tunayoyasimamia. Sheria ya kazi si ya upande mmoja. Inapowekwa kwa usawa inaleta heshima, ufanisi, na mshikamano kazini, ATE itaendelea kusimamia hilo kwa nguvu zote.” Suzanne Ndomba

Aidha, ameiomba Serikali kufikiria kupunguza tozo ya maendeleo ya ujuzi kutoka asilimia 3.5 hadi asilimia 2, akieleza kuwa licha ya kuelewa dhamira ya Serikali kuhusu tozo hiyo, bado imekuwa mzigo kwa baadhi ya waajiri.

“Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeendelea kuboresha huduma zake, hususan kupitia matumizi bora ya TEHAMA yaliyofikia zaidi ya 93%. Kufikia Julai 1, 2025, tutatimiza miaka 10 ya kutoa huduma, na tunaichukulia kama fursa muhimu ya kufanya tathmini ya kina ya huduma zetu zote kwa lengo la kujiboresha zaidi. Katika maadhimisho haya, tunapenda pia kutangaza kuwa WCF inaanzisha Fao la Utengamavu na Fao la Ujuzi Mbadala, kama sehemu ya maboresho yanayolenga kuwahudumia wafanyakazi kwa ufanisi zaidi.” – Dk. Omary, Mwakilishi wa WCF

“Ikiwa mwajiri ana malengo mbalimbali kama kuongeza faida, basi mfanyakazi naye ana nafasi muhimu ya kuchangia kuyafikia. Hii ndiyo sababu msingi wa UTATU — baina ya mwajiri, mfanyakazi, na serikali — ni wa muhimu sana katika kujenga mazingira bora ya kazi. Nipende kuwasihi waajiri waendelee kusimamia haki, sheria, pamoja na miongozo iliyowekwa ili kuendeleza utatu huu na kufikia malengo ya kila mmoja wetu.” – Rehema Ludanga, Naibu Katibu Mkuu TUCTA