RC Chalamila, JUMAKITA pamoja kwa futari

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 03:14 PM Mar 23 2025
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akimpa sadaka mmoja wa wanawake waliofika katika hafla ya ugawaji futari
PIcha: Pilly Kigome
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akimpa sadaka mmoja wa wanawake waliofika katika hafla ya ugawaji futari

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amegawa sadaka ya futari kwa wanawake zaidi ya 600 wenye mahitaji maalum kutoka Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA), kuwawezesha kujikimu chakula katika kipindi cha mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mbali na hilo, ameagiza jumuiya hiyo kutumia hekma, busara na akili kubwa, ili kuweza kufikia malengo sahihi bila kuleta athari katika jamii hasa katika swala zima la kuongeza familia.

Ameyasema hayo leo, Machi 23, 2025 jijini Dar es Salaam, Makao Makuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) katika ugawaji sadaka ya futari kwa wanawake wenye uhitaji.

Mufti Mkuu wa Tanzania Abubakar Zuber akizungumza na wanawake wa Juwakita Makao Makuu ya Bakwata
Amesema wanawake wanatakiwa watafakari kwa kina kabla ya kuchukua maamuzi, ili kuepukana na changamoto za maisha ya usoni hususani katika vizazi vijavyo.

"Nyinyi wanawake mkisimama imara kama inavyotakiwa katika suala zima kufanya chaguzi na mtu ambae unaenda kuanzisha mahusiano basi naamini hili swala la watoto wa mitaani tutakwenda kulimaliza kwa asilimia mia," amesema.

Aidha amesema ugawaji futari umekuja baada ya kuona umuhimu mkubwa kuwagawia futari  wanawake ambayo haijapikwa wakafuturu na walio nyuma yao wanaowategemea kuliko kuwaita mahali wafuturu wao pekee na nyumbani wameacha watoto na wanaowategemea.

Wanawake kutoka JUWAKITA Mkoa wa Dar es Salaam katika viwanja vya Bakwata waliofika kugawiwa sadaka ya futari
Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi, amewataka wanawake hao katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kuepukana na fitina, unafiki, uongo, uchonganishi ili kuvuka salama kipindi hicho.

Mufti amesema kuwa katika kipindi hicho kijacho cha uchaguzi kutazuka mambo mengi wasiyoitakia mema nchi na kuweza kupenya kwenye makundi na Jumuiya za wanawake, ili mradi kukosesha amani ya nchi.

"Nawausia akinamama achaneni na uzishi uzushi kwakuwa kipindi hiki wanafiki watu waongo waongo machawa watazuka sana kuwatumia ninyi wanawake kuishi kwa tahadhari kubwa kuendelea kuilinda amani yetu ya nchi," amesema Mufti.

Wanawake kutoka JUWAKITA Mkoa wa Dar es Salaam katika viwanja vya Bakwata waliofika kugawiwa sadaka ya futari
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amewakumbusha wanawake hao waende wakajiandikishe katika daftari la kudumu la mpigakura, ili waweze kushiriki katika uchaguzi mkuu kuchagua viongozi wanaowataka.

Amesisitiza wanawake ni jeshi kubwa nchini, hivyo wasimame na kwenda kuchagua viongozi makini wa kuisogeza nchi mbele.