RC Mara aagiza msako wa Mbunge Kajege kwa kukwepa vikao

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:59 PM Mar 05 2025
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtamb
PICHA: MWANDISHI WETU
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtamb

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo, Gerald Kusaya kufuatilia ili kujua aliko Mbunge wa Mwibara wilayani Bunda, Charles Kajege kwa kukosekana kwa muda mrefu kwenye vikao muhimu vya maendeleo ya wananchi.

Akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara kilichofanyika mjini Musoma jana, Kanali Mtambi alisema mbunge huyo hajaonekana kwenye vikao vya mkoa vinavyojadili maendeleo ya wananchi kwa mwaka mzima sasa.

Kanali Mtambi alikosoa utendaji wa Kajege, alioutafsiri tofauti na wabunge wengine ambao wamekuwa wakifika mara kadhaa kwa ajili ya kujadili maendeleo ya wananchi na hivyo kuamuru kutafutwa kwa Mbunge huyo.

“Mheshimiwa Kajege, sijui yuko mkoa gani, mwaka mzima. Kuna wabunge hapa zaidi ya mara kumi wamekuja kwa masuala ya wananchi, tunazungumza, tunajadiliana, tunashauri na tunakimbiza masuala ya wananchi, lakini mwaka mzima, eee! Au anaumwa?” alihoji Kanai Mtambi na kuagiza atafutwe.

Aliongeza: “RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) hebu jaribu kufuatilia tujue mheshimiwa mbunge ana tatizo gani ili tuone kama taratibu zinaturuhusu wakati wa vikao muhimu hivi ambavyo wananchi wanahitaji uwakilishi tuone namna ya jimbo hilo kuwa na uwakilishi badala ya yeye, kwa sababu sasa wananchi wanawakilishwa na nani kwenye jimbo hilo.”

Aidha, Mkuu wa Mkoa aliuomba uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa kuisaidia serikali kumtafuta Kajege huku akisisitiza umuhimu wa wabunge kuzingatia wajibu wao wa kuwakilisha wananchi kwenye vikao vya maamuzi ya kimaendeleo.

“Menyekiti wa Chama mtusaidie mambo haya, na niendelee kusisitiza kuwa kazi ya mwakilishi ni kuwakilisha wananchi katika vikao hivi vya kimaamuzi na kisheria, wengine tumejadiliana mambo ambayo wanahitaji yafanyike kwenye majimbo yao, lakini huyo [Kajege] mwaka mzima haonekani,” alisema Kanali Mtambi.