Samia ataka polisi kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani kuelekea uchaguzi

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 05:39 PM Jun 09 2025
Rais Samia Suluhu Hassan

Rais Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi la Polisi kudhibiti vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Aidha, amelitaka jeshi hilo kuwekeza nguvu zaidi katika kudhibiti ajali za barabarani, akibainisha kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na ajali hizo kwa mwaka huu ni kubwa.

Rais Samia alitoa maagizo hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akihitimisha mafunzo ya maafisa na wakaguzi wasaidizi wa Jeshi la Polisi, mafunzo ambayo yalianza mwaka jana.

Amesema ameanza kuona mabadiliko makubwa ndani ya Jeshi la Polisi, hususan katika masuala ya nidhamu, utendaji kazi, na kupungua kwa manung’uniko kutoka kwa wananchi.