RIPOTI ya utafiti kuhusu afya ya akili imebaini vijana wa kitanzania wana ustahimilivu mkubwa wa akili, wakipata alama za juu katika ustawi eneo hilo kati ya nchi 76 zilizofanyiwa utafiti duniani.
Miongoni mwa sababu za vijana wa Tanzania kuwa imara katika afya ya akili ni kiwango kidogo cha matumizi ya vyakula vilivyosindikwa.
Utafiti uliofanywa na taasisi ya Sapien Labs kuhusu Afya ya Akili Duniani 2024, unaonesha kuwa pamoja na vijana kupata alama za juu duniani, viwango vya vijana wa Tanzania, bado viko chini kulinganishwa na wastani wa watu wazima wa rika kubwa duniani. Katika nchi zote, vijana wana afya ya akili duni kulinganisha na vizazi vya zamani.
Ni katika nchi 15 pekee kati ya 76 ambapo wastani wa MHQ kwa vijana ulizidi 50, na ni nchi moja tu – Tanzania – ambayo wastani wa MHQ ulizidi 65, sawa na wastani wa chini kabisa kati ya watu wa miaka 55 na zaidi katika nchi nyingine.
Ripoti hiyo ambayo imehusisha washiriki milioni moja ambao ni watu wanaotumia mtandao katika nchi 76 kwenye mabara yote, inaonesha kuwa Tanzania ni nchi pekee ambayo wastani wa Kipimo cha Afya ya Akili (MHQ) kwa vijana wanaotumia mtandao unazidi 70.
Utafiti pia umebaini takwimu hizo zinatofautiana sana na mataifa ya Magharibi, ambako afya ya akili ya vijana imeshuka kwa kasi tangu mwaka 2019 bila kuwapo dalili za kuimarika. “Kuporomoka huku kwa afya ya akili duniani kunahusishwa na kupungua kwa uwezo wa kudhibiti na kuhimili mawazo na hisia pamoja na ugumu wa kujenga na kudumisha uhusiano chanya na watu,” inabainisha ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu wazima wa rika kubwa duniani kote walipata wastani wa 100 MHQ, huku nchi zilizo na viwango vya juu zaidi vya afya ya akili kwa wazee (zaidi ya alama 110), zikijumuisha mataifa ya Afrika, Amerika ya Kati na Kusini, Kusini Mashariki mwa Asia, Israel, na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Kwa upande wa vijana walio na umri chini ya miaka 35, wastani wa MHQ kwa nchi 76 uko kati ya tano hadi 71, huku wastani wa dunia ukiwa 38, zaidi ya alama 60 chini ya watu wenye umri wa miaka 55 na zaidi. Pia utafiti umebaini idadi kubwa ya vijana chini ya miaka 35 wanaishi kwa tabu, huku asilimia 41 wakiorodheshwa kama wenye msongo mkubwa wa mawazo au matatizo makubwa, wakikumbana na angalau dalili tano au zaidi za matatizo ya akili yanayowaathiri kwa kiwango kinachowafanya washindwe kuendesha maisha yao kwa ufanisi.
Mwanzilishi na Mwanasayansi Mkuu wa Sapien Labs, Dk. Tara Thiagarajan, anasema: “Afrika ina faida ya kipekee katika afya ya akili ya vijana, rasilimali ambayo lazima ilindwe kwa makini wakati bara hili linapitia mabadiliko ya kasi ya kiteknolojia na kiuchumi.
“Kwa kuwa idadi ya vijana barani Afrika inatarajiwa kuwa na nafasi muhimu katika uchumi wa dunia katika miongo ijayo, serikali zinapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha ukuaji wa miji, matumizi ya teknolojia ya kidijitali na mabadiliko ya mtindo wa maisha, hayadhoofisha ustahimilivu wa akili, ambao kwa sasa unawafanya vijana wa Afrika kuwa wa kipekee duniani,” anashauri.
Ripoti inataja sababu zilizobainika kuwa chanzo cha ustahimilivu wa akili kwa vijana wa Tanzania na kuwa na viwango vya juu vya afya ya akili, ikiwamo kiwango kidogo cha matumizi ya vyakula vilivyosindikwa kupita kiasi. Pia sababu nyingine ni hatua ya Tanzania kupiga marufuku matumizi ya plastiki zisizokubalika kiafya, ambazo husababisha sumu.
Utafiti unataja sababu zaidi za mafanikio hayo kwa Tanzania kuwa ni matumizi madogo ya simu janja miongoni mwa watoto, ikitajwa kuchangiwa na usambazaji duni wa mtandao nchini. Utamaduni wa kijamii unaothamini mshikamano wa kifamilia na urafiki zaidi kuliko maisha ya kifahari pia unatajwa kuwa na manufaa kwa Tanzania.
Hata hivyo, watafiti wanaonya kuwa kadri Afrika inavyoendelea kujikita katika miji na kutumia zaidi teknolojia, faida hizi zinaweza kupotea na kusababisha kushuka kwa afya ya akili ya vijana barani kote. Dk. Thiagarajan anaongeza: “Ripoti hii inaonesha pengo kubwa kati ya vizazi katika afya ya akili duniani.
Wakati watu wazima wa miaka 55+ wanaendelea kuwa na afya ya akili bora, vijana wanakabiliwa na msongo wa mawazo kwa viwango vya kutisha. “Athari ya hili ni kwamba tunapopoteza kizazi cha zamani kutoka katika nguvukazi, kizazi kipya huenda kisiweze kukabiliana na shinikizo la maisha ya kila siku. “Hii inaweza kusababisha kupungua kwa tija, ongezeko la kutokuwapo kazini, ushirikiano mdogo, msongo wa mawazo mkubwa na hata ongezeko la vurugu katika maisha ya kila siku kutokana na ukosefu wa uwezo wa utambuzi wa kukabiliana na changamoto.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED