SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Nigeria imefanya kongamano kubwa la uwekezaji nchini humo lengo ikiwa ni kuvutia wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali ndani ya Afrika.
Kongamano hilo ambalo lilifanyika kwenye miji ya Lagos na Enugu lililenga kuwaeleza wawekezaji wa Nigeria fursa mbaliambali za uwekezaji zinazopatikana hapa nchini.
Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Mwenyekititi wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Dk. Binilith Mahenge.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Dk. Mahenge, alielezea mageuzi makubwa ambayo Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan ameyafanya na kuvutia uwekezaji kutoka nje.
“Katika kukuza diplomasia ya uchumi serikali ya Tanzania imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara na hali hiyo imewavutia wawekezaji wengi kutoka mataifa mbalimbali,” alisema Dk. Mahenge
Kongamano hilo lilijadili kuhusu sekta ya uzalishaji viwandani, ujenzi wa majengo, utalii, dawa, uchumi wa buluu, misitu, mifugo, huduma za kifedha, mafuta na gesi na uchakataji wa mazao ya chakula.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED