"Tunahakikisha maendeleo ya wanawake yanapewa msukumo" – Dk. Gwajima

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:40 PM Mar 04 2025
Waziri wa Maendeleo ya Jamii,  Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Doroth Gwajima  (katikati), akisalimiana na Mkuu wa Kitengo cha Biashara  wa Benki ya Stanbic Tanzania, Peter Bitesigilwe, wakati akiwasili.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Doroth Gwajima (katikati), akisalimiana na Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Benki ya Stanbic Tanzania, Peter Bitesigilwe, wakati akiwasili.

Benki ya Stanbic Tanzania imedhamini Kongamano la Maendeleo ya Wanawake lililofanyika katika Halmashauri ya Ushirombo, mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea kilele cha Wiki ya Wanawake.

Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, alieleza kuwa lengo la mkutano huo ni kutambua mchango wa wanawake wa mkoa wa Geita na Tanzania kwa ujumla katika maendeleo ya taifa.

"Kongamano hili ni moja ya matukio kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika kitaifa jijini Arusha, yakiongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan," amesema Gwajima.

Ameongeza kuwa maendeleo ya wanawake yanapaswa kupewa msukumo unaostahili ili kuhakikisha ushiriki wao kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa taifa. Aidha, ameishukuru Benki ya Stanbic kwa kuwezesha kongamano hilo na kuzitaka taasisi nyingine za kifedha kuiga mfano huo.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Idara ya Biashara wa Stanbic Tanzania, Fredrick Max, amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imekuwa ikisisitiza kuwa jukumu la kuwainua wanawake ni la kila mmoja—serikali, sekta binafsi, na wadau wa maendeleo.

"Sisi, Benki ya Stanbic, tunatekeleza azma hii kwa vitendo kwa kutoa mikopo nafuu inayowalenga wanawake na vijana. Kupitia kauli mbiu ya mwaka huu, 'Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji,' tumeanzisha programu maalum kama Ignite Women inayolenga kuwawezesha wanawake kujiamini na kuongoza," amesema Max.

1

Ameongeza kuwa Stanbic inaendelea kukua kwa kasi, ikiwa ni benki ya tatu kwa ukubwa nchini kwa mujibu wa ripoti ya kifedha ya mwaka 2024. Benki hiyo inaendelea kusaidia miradi mikubwa ya kimkakati ya taifa, ikiwa na matawi 11, huku sita yakiwa mbioni kufunguliwa mwaka huu, ikiwemo moja mkoani Geita.

Akihitimisha kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela, ameishukuru Benki ya Stanbic kwa mchango wake katika kuwawezesha wanawake na jamii kwa ujumla.

"Tunaishukuru Benki ya Stanbic kwa ushirikiano wake na namna ilivyowezesha kongamano hili. Ni wazi kuwa benki hii inajishughulisha kwa kiwango kikubwa na maendeleo ya wanawake," amesema Shigela.

Kongamano hilo limewaleta pamoja wadau mbalimbali wa maendeleo, wanawake wajasiriamali, na viongozi wa serikali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha juhudi za kuwawezesha wanawake kiuchumi.