Kanisa la Mlima wa Moto la Mikocheni jijini Dar es Salaam, limeendelea kuenzi kazi nzuri zilizokuwa zikifanywa na mwasisi wake Hayati Askofu Dk. Getrude Rwakatare ikiwemo kuombea amani ya nchi na viongozi wake.
Hayo yalisemwa jana Jumapili na Askofu wa Kanisa hilo, Rose Mgeta wakati wa tamasha la kuadhimisha miaka mitano tangu mwasisi wa Kanisa hilo Dk Getrude Rwakatare afariki dunia.
Alisema kila mwaka wamekuwa wakifanya tamasha kubwa kama hilo kuenzi kazi za mwasisi wake ikiwemo kuliombea taifa na viongozi wake.
“Kanisa hili ni maono ya Askofu wetu mwanzilishi hayati Askofu Dk. Getrude Rwakatare na tumekuwa tukiyaendeleza maono yake mwaka hadi mwaka na makanisa yote ya Mlima wa Moto wamekuwa wakifanya maombi haya kila mwaka,” alisema
Alisema kanisa hilo litaendelea kuombea taifa liendelee kuwa na amani na kuondokana na majanga kama ukame, mafuriko na matatizo mbalimbali yanayotokea kwenye jamii.
“Ili Kanisa liwe na amani lazima nchi iwe na amani kwa hiyo umekuwa wajibu wetu kuhakikisha tunaombea amani ya nchi mara kwa mara na tunamuombea Rais wetu Mungu aendelee kumpa afya njema aweze kuendelea kulikongoza vyema taifa letu,” alisema Askofu Rose
Alisema Askofu Dk. Getrude Rwakatare aliweka misingi mizuri ya Kanisa na ndiyo sababu limekuwa likiendelea kutoa huduma ya kiroho hata baada ya kuondoka kwake.
Mtoto wa Hayati Dk Rwakatare, Dk Kellen-Rose Rwakatare alisema wamekuwa wakifanya tamasha kila mwaka kanisani hapo kama sehemu ya kuenzi kazi nzuri za mwanzilishi huyo katika jamii.
Dk Kellen-Rose ambaye ni Mwenyekiti wa Wazazi (CCM), Morogoro alisema maono ya mama yake yote aliyokuwa akiyasimamia zikiwemo shule za msingi na sekondari zimeendelea kufanya vizuri hata baada ya kuondoka kwake duniani.
“Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya mama yetu, Hayati Mchungaji Dk Getrude Rwakatare na sisi tuliobaki tumejitahidi kwa uwezo wetu kusimamia maono yake na tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa kusimamia misingi aliyoiweka,” alisema Dk Kellen-Rose.
“Namshukuru Rose Mgeta kwa kusimamia maono haya na kuhakikisha kazi ya Mungu inaendelea na nashukuru kwa mzigo mkubwaa alionao Rose kuombea taifa hili ni watu wachache wanaojitoa kuombea taifa lakini Rose na kanisa wamesimama kuombea nchi dhidi ya majanga kama ukame,” alisema
Alisema mbali na kuwa mwanzilishi wa Kanisa la Mlima wa Moto la Mikocheni B jijini Dar es Salaam, Hayati Dk Getrude Rwakatare ni mwanzilishi wa shule za Kimataifa za St Mary’s ambazo ziko kwenye mikoa mbalimbali nchini na zimeendelea kufanya vizuri kila mwaka.
Hadi anafariki Aprili 20 mwaka 2020, Dk Getrude Rwakatare alikuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Morogoro na mjasiriamali aliyeanzisha biashara mbalimbali.
Kabla ya kufariki dunia Dk Rwakatare alianzisha utaratibu wa kutembelea mahabusu na wafungwa kwenye magereza na kuwatoa watu waliokosa dhamana, alisomesha watu mbalimbali na aliwapa mitaji ya biashara wajasiriamali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED