Wakazi wa Kijiji cha Kolagwa, Kata ya Tengelea, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wamemshukuru Diwani wao Shabani Manda kwa juhudi zake zilizopelekea kujengwa kwa kituo cha afya katika kijiji hicho.
Shukrani hizo zilitolewa na wananchi mara baada ya uzinduzi wa kituo hicho cha afya, ambao umeleta afueni kubwa kwao kutokana na miaka mingi ya kukosa huduma hizo muhimu kijijini kwao.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwajuma Juma alisema kuwa kwa muda mrefu walikuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya katika maeneo ya Hoyoyo au Mkuranga.
"Kutoka Kolagwa kwenda Hoyoyo au Mkuranga unahitaji kutumia shilingi 10,000 kwa bodaboda kwenda na kurudi. Sio kila mmoja ana uwezo huo, na wengi walikuwa wakishindwa kuhudhuria kliniki au kuwapeleka watoto kupata chanjo zote," alisema Mwajuma.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa kituo hicho kijijini kwao utawapunguzia gharama kubwa za usafiri na kuwahakikishia huduma bora karibu na makazi yao.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Tengelea, Shabani Manda, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ameweza kusimamia ujenzi wa zahanati tatu katika kata hiyo.
Katika uzinduzi wa zahanati hiyo, Manda aligharamia matibabu ya siku hiyo kwa wakazi wote wa kijiji hicho.
"Leo tunafungua zahanati yetu, na nimeamua kugharamia matibabu ya siku hii kwa wote wenye uhitaji," alisema.
Manda aliongeza kuwa huduma katika zahanati hiyo zitaendelea kutolewa kwa gharama nafuu, huku wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, na wazee wakitibiwa bure kwa mujibu wa msamaha wa serikali.
Aidha, alimshukuru Vikundi vya Jirani kwa Jirani (VJK) kwa kuanzisha ujenzi wa zahanati hiyo hadi hatua ya kozi ya nne, na kuongeza kuwa ujenzi wa kozi zilizobaki hadi kukamilika uligharimu shilingi milioni 50, zilizotokana na ofisi ya kijiji pamoja na nguvu kazi ya wananchi.
Pia alimpongeza mwekezaji Christopher Lema kwa msaada wake katika kufanikisha ujenzi huo.
Katika salamu zake za shukrani, Manda alimsifu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sekta ya afya na kuhakikisha jamii inapata huduma bora za kijamii.
Amesema atahakikisha ndani ya wiki mbili zahanati hiyo inapata huduma ya umeme kwa gharama zake binafsi ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Mohamed Mahudu, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, alimmiminia pongezi Manda kwa kazi kubwa ya maendeleo katika kata yake.
"Katika kipindi cha miaka mitano, Manda ameweza kujenga zahanati tatu. Hii ni kazi kubwa inayostahili pongezi," alisema Mahudu.
Aliongeza kuwa halmashauri italifanyia kazi suala la kukosekana kwa nyumba ya mganga katika zahanati hiyo, ili kuhakikisha huduma bora zinaendelea kutolewa kwa wananchi wa Kolagwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED