Wasira, ataka wanachama kuwafikishia wananchi utekelezaji wa Ilani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:40 PM Mar 24 2025
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, amewataka wanachama wa chama hicho kuwafikishia wananchi taarifa za mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza kwenye mkutano wa ndani wa wanachama wa CCM uliofanyika jana Jumapili, Machi 23, 2025, katika Wilaya ya Karagwe, ambao uliwahusisha pia viongozi wa Wilaya ya Kyerwa, Wasira aliwataka wanachama wa chama hicho kuwaeleza wananchi miradi na maendeleo yaliyofanikishwa na serikali.

"Nawaomba muende kwa wananchi na muwaeleze haya wanayoyaona ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Msione zahanati zimejengwa, magari ya kubeba wagonjwa yamepatikana, madarasa yamejengwa, mkumbuke yote haya ni kazi ya Rais Samia. Nendeni mkawaambie wananchi," alisema Wasira.

Aliwasisitiza wanachama wa CCM kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi kuelewa kazi kubwa inayofanywa na serikali katika kuboresha huduma za jamii na miundombinu ili kuhakikisha maendeleo endelevu kwa Watanzania.