Wasira: Kagera fugeni ng'ombe mpate fedha za kujikimu

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 05:35 PM Mar 23 2025
news
CCM
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara, Stephen Wassira akizungumza na wananchi katika Viwanja vya Kemondo,mkoani Kagera

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amewataka wananchi mkoani Kagera kutumia rasilimali zilizopo mkoani humo ikiwemo mifugo ya ng'ombe ili kujiinua kiuchumi.

Amebainisha hayo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Kemondo Center ndani ya Tarafa ya Katerero Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.

 "Kama familia zinaweza kufanya ufugaji wa ng,ombe kila kaya hata ng'ombe wawili  hizo familia zikawa na uhakika wa kupata maziwa na kikawepo kiwanda cha maziwa familia zinaweza kupata pesa na kujiokoa na umasikini," amesema Wasira.

 

PICHA: CCM
Aidha, Wasira amesema chama hicho kunatambua kuwa Mkoa wa Kagera unazungukwa na  ziwa na  mito mikubwa hivyo vijana wanaweza kufanya ufugaji wa samaki wa vizimba, na ufugaji huo unaweza kuwaingizia fedha za haraka.

Kadhalika, Wasira amesema serikali imetoa Sh.bilioni 106.4 kufanikisha miradi ya maji, afya, barabara, umeme na elimu katika Jimbo la Bukoba Vijijini mkoani Kagera kwa kipindi cha miaka minne.

Amesema kupitia  Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) itaendelea kujenga vyuo hivyo kila wilaya ili kuendelea kutoa uzoefu kwa vijana wengi Mkoa wa Kagera kuendelea kujiajili na kuajiliwa huku akiwataka viongozi waliopewa dhamana na wananchi wao kuendelea kufanya ubunifu  wa kuwangunisha katika mifumo ya kuwapatia vijana pesa ya haraka kama mifugo na uvuvi.