HALMASHAURI ya Manispaa ya Ubungo, inatarajia kutumia Sh. Bil.2.4 kwa mapato ya ndani kuwapatia mikopo ya asilimia kumi kwa vikundi vipatavyo 90 kwa Wanawake, Vijana na Walemavu.
Hayo yamesemwa leo, Machi 6, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Lazaro Twange, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, katika hafla ya kuwapatia hundi wawakilishi wa vikundi hivyo iliyofanyika katika viwanja vya halmashauri hiyo.
Amesema fedha hizo zitatolewa kwa vikundi vilivyotimiza vigezo baada ya mikopo hiyo, kurejeshwa awali jumla ya vikundi 209 viliomba mkopo na vilivyofanikiwa kutimiza vigezo ni vikundi 90.
Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Manispaa Ubungo, Kissa Mbila amesema Halmashauri imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali katika kuendesha mfuko wa uwezeshaji wa vikundi, ikiwamo wanakikundi kutokurejesha marejesho kwa wakati na kufanya fedha nyingi kuwa mikononi mwa wakopaji.
Baadhi ya vikundi kusambaratika, kuhamahama kwa wanufaika, migogoro baina ya wanakikundi hasa baada ya kuingiziwa fedha na kushindwa kutekeleza miradi.
Pamoja na vikundi kutowekeza fedha zote za mkopo kwenye miradi waliyoomba na badala yake wanagawana fedha kwa matumizi binafsi na kushindwa kukuza miradi ya vikundi na kushindwa kufanya marejesho kulingana na mkataba.
Amesema halmashauri wana mpango mkakati wa kuwachukulia hatua za kisheria vikundi hivyo, ili waweze kurejesha na wengine wanufaike.
Meya wa Ubungo, Jafari Nyaigesha, alitoa maelekezo kwa makundi wanufaika kuwambia fedha hizo wanazopewa sio zawadi na hawapewi kwenda kufanya shughuli zao binafsi ambazo sio za kuwainua kuichumi na kudhani hazitakiwi kurudi jambo ambalo sio kweli wasijidanganye.
"Fedha hizi ambazo mnaenda kunufaika sio zawadi akina mama na wala hatuwaambii muende mkatunzane na mashoga zenu kwenye vigodoro ni lazima zirudishwe," amesisitiza Meya.
Vikundi vya mfano vilivyopokea hundi kikiwemo kile cha Vijana cha Ubungo kimepata mkopo wa Sh. Mil.60, Kikundi cha Rise cha Kata ya Kimara na Elibea kutoka Kata ya Mbezi vilikuwa vikundi vya mfano.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED