WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amesema taasisi za umma na za binafsi hazina haja tena ya kuwekeza katika mifumo yao, badala yake wakitumie Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC) kuhifadhi taarifa zao.
Ameyasema hayo katika ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alipotembelea kituo hicho kilichoko Kijitonyama, mkoani Dar es Salaam, kujionea namna Mfumo wa N- CARD unavyofanya kazi.
Silaa amesisitiza umuhimu wa taasisi hizo kuwekeza katika kituo hicho ili kupata huduma salama na kwa gharama nafuu. "Lengo Kuu la Waziri Mkuu ambaye ameongozana na viongozi mbalimbali ni kushuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana
Kupitia Uwekezaji wa serikaliI katika TEHAMA," amesema Silaa.Amesema kwa sasa serikali inaendelea na mchakato wa kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kupitia Kadi Moja ya Jamii itakayounganishwa na taarifa zao za NIDA.
"Kadi hiyo itarahisisha miamala ya kifedha na itatumika katika huduma mbalimbali vikiwapo viingikii kwenye viwanja vya mpira, vivuko, usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), taasisi za kifedha na maeneo mengine muhimu,"amesema Silaa.
Amesema mradi wa Digitali Tanzania ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Kadi Jamii unaendelea kutekelezwa kwa lengo la kuhakikisha mifumo yote ya taasisi mbalimbali inasomana, ili kuwezesha utoaji wa huduma kwa ufanisi.
Amesema katika bajeti ya mwaka 2024/2025, serikali ilitenga Sh. bilioni 10 kuiwezesha NIDC kuimarisha shuguli zake zikiwamo zinazotekelezwa kupitia mradi huo wa kidijitali.
"Kupitia mradi huu, wananchi wataweza kutumia Kadi Jamii yenye kuunganishwa na namba yao ya NIDA kufanya miamala yote ya kifedha na manunuzi, hivyo kuondoa hitaji la kubeba kadi nyingi,"amesema Silaa.
Amesema hatua hiyo inalenga kumrahisishia mwananchi maisha ya kila siku kwa kumwezesha kutumia kadi moja tu kwa huduma mbalimbali. Amesema serikali iko katika mkakati wa kuhakikisha kila mwananchi anamiliki simu janja kwa gharama nafuu ili kuitumia sambamba na kadi hiyo.
Akizungumzia kuhusu Mkongo wa Taifa unaosimamiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri huyo amesema tayari umeunganisha wilaya 109 kati ya 139 na baadhi ya nchi jirani za Afrika zimeunganishwa, hatua ambayo itaongeza ufanisi na kupanua huduma za kidijitali nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED