Bagamoyo 'kuchele' kibandari, kazi

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 09:17 AM Feb 28 2025
Katuni
Mchoro: Muhidin Msamba
Katuni

RAIS Samia Suluhu Hassan ana ziara ya kikazi mkoani Tanga, ambako anasema serikali inajenga Bandari ya Bagamoyo na kongani kubwa ya viwanda, ili kufungua uchumi wa mikoa yote ya ukanda wa Pwani.

Mikoa mingine ya ukanda huo ni Tanga ambako anasema serikali itajenga Bandari ya Uvuvi Pangani, kiwanda cha sukari wilayani Pangani na soko kubwa la kimataifa la samaki. 

Mbali na hilo, anasema serikali inatarajia kuimarisha miundombinu ili kurahisisha usafiri na usafirishaji bidhaa kuanzia mpaka wa Horohoro, Pangani -Tanga hadi mikoa ya Lindi na Mtwara. 

Aidha, anasema mbali ya Bandari ya Bagamoyo, kongani kubwa ya viwanda itaongeza ajira, kuchochea biashara na ukuaji wa sekta zingine, ikiwamo ya utalii. 

Kwa maelezo hayo ya Rais ni wazi kwamba wakazi wa Bagamoyo na mikoa ya ukanda wa Pwani, wajiandae kuchangamkia fursa  za ajira zitakazopatikana kutokana na ujenzi wa bandari, huku wakiwa na sura mbili; kicheko kwanza, kisha ‘hapa kazi tu hadi kieleweke’ . 

Kwa kuwa inaelezwa na Rais mwenyewe kuwa, kujenga kongani ya viwanda Bagamoyo na ujenzi wa bandari, ni hatua kubwa itakayounganisha mji huo mkongwe, ni hatua kubwa ya kuunganisha Tanga na mji huo wenye historia kubwa ya nchi hii enzi za utumwa. 

Nadhani wakati wa ujenzi wa bandari ukiendelea, ziwepo pia juhudi za kupanua barabara, ili kurahisisha usafiri kutoka ndani ya Bagamoyo na nje, ili iwe rahisi watu kutoka maeneo mbalimbali kwenda kufanya shughuli zao ndani ya mji huo mkongwe na kurudi katika makazi yao. 

Kwa mfano, kumekuwapo na changamoto ya foleni za magari kutoka na kuingia mjini humo, Dar es Salaam kwenda mjini Bagamoyo ambazo wakati mwingine husababishwa na ufinyu wa barabara na kuwafanya watu kuchelewa katika shughuli zao za kila siku. Iwapo changamoto hiyo itapatiwa ufumbuzi, ninaamini Bagamoyo kutakucha, kwa kuwa watu wanaofika huko kwa ajili ya utalii, biashara na kufanya shughuli mbalimbali watakuwa na uhakika wa usafiri. 

Kwa kuwa lengo la serikali ni kuufungua ukanda wa Pwani kuanzia mikoa ya kusini hadi katika mpaka wa Horohoro kuelekea Mombasa, Kenya, basi wadau wa maendeleo wahusike kufanikisha. 

Ahadi ya Rais ni kujenga daraja la Pangani mkoani Tanga na barabara ya kilometa 256 kwa kiwango cha lami, ili kuifungua na kuunganisha Pangani na shoroba za kiuchumi. Ninaunga mkono juhudi hizo, ila nikiendelea kuongeza kuwa upanuzi wa barabara ya kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo kunakojengwa bandari kutasaidia kupunguza foleni za magari zisizo za lazima. 

Ikumbukwe kuwa kuna watumishi wanaofanya kazi Bagamoyo wanaishi Dar es Salaam, wengine wanafanya kazi Dar es Salaam wanaishi Bagamoyo, pia wapo wanaofanya biashara Dar es Salaam wanaishi Bagamoyo au kufanya biashara Bagamoyo wanaishi Dar es Salaam. 

Kwa maana hiyo, kuna wasafiri wa kila siku wanaotoka Bagamoyo na kuingia Dar es Salaam au kutoka Dar es Saalam kuingia Bagamoyo, hivyo, suala la kuwapo kwa usafiri usio na usumbufu ni muhimu. Barabara kubwa inayopitika wakati wote ni suluhisho la changamoto ya foleni zinazotokana na ufinyu wa barabara kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo au kutoka Bagamoyo hadi Dar es Salaam. 

Watumiaji wa Barabara ya Bagamoyo watakuwa wanajua adha wanazokutana nazo kila siku hasa wakati wa jioni. Hivyo, uamuzi wa serikali wa kuongeza fursa za kiuchumi, uwashtue wajenzi wa barabara kuchukua hatua ya kuipanua mapema.