HADI sasa katika jamii, kuna vilio vya mabinti kushiriki utoaji mimba, tena wakitumia njia zisizo sahihi kiafya na kisheria. Ni dhana ngumu inayowafanya mabinti kutafuta njia mbadala wa kutoa mimba zisizotarajiwa.
Mtaalamu bingwa wa tiba ya kinamama, Dk. Elias Kweyamba, anarejea matokeo ya utafiti mojawapo mwaka 2016, yalionyesha kila mwaka kuna kundi kubwa la wanawake wanaotumia njia potofu kutoa mimba zisizotarajiwa. Hiyo ni kutokana na sheria kukataza nchini.
Kwa mujibu wa Dk. Elias Kweyamba, vifo vitokanavyo na uzazi usio salama, zinachangia hadi matukio ya vifo, kwa sababu ya kukosekana uelewa kuhusu uzazi salama.
Watafiti wanaainisha kila mwaka kuna kundi kubwa la wanawake nchini wanaopata mimba zisizotarajiwa na daktari huyo anataja takwimu, wengi ni mabinti wenye umri kati ya miaka 15 na 19.
Hapo ana ufafanuzi kwamba wengi ni kutokana na umri mdogo wanashindwa kuamua kwa busara, azma ya kubaki kwenye afya salama na inaelezwa hadi sasa, idadi kubwa ya mabinti hao ni wanafunzi wa ngazi tofauti kielimu.
Inaelezwa kuwa, rika hiyo inaangukia njia potofu za utoaji mimba, hata wanakumbwa na madhara kiafya, hasa katika mfumo wa uzazi wanatokwa na damu nyingi, pia kukiwapo ushuhuda wa matukio ya vifo kwa wahusika, wengine wanakwama kutekeleza malengo yao kimaisha.
Kweyamba anataja njia hizo zinazoripotiwa kutumika kutoa mimba, zinajumuisha miti ya mihogo, dawa ya kung’arisha mashati (blue), spoku za baiskeli, majani ya chai, pia majivu zinatajwa na madaktari, ukiwa ni uzoefu wao kutoka kwa wajawazito wengi wenye matatizo wanapowafikia.
Mbinu nyingine inayoripotiwa katika utoaji mimba huo wa kujitegemea, mtaalamu huyo anagusa matumizi ya dawa inayofanana na vichocheo vya mwili, yaani ‘misoprostoli’. Vilevile anasema kuna uingizaji vifaa visivyo vya kiupasuaji kama sindano za tiba.
Kihistoria idadi ya mimea inayotumiwa kutoa mimba, ndio imetumika pia katika utabibu, japo si njia sahihi zinazomfanya mama abaki salama kiafya, moja ya vigezo vikuu ni vipimo vya matumizi ya dawa hizo kutokuwa sahihi.
Dk. Kweyamba anaainisha eneo lingine la madhara ya mbadala huo, ni uwezekano wa kusababisha madhara kama vile akili, ukitokana na msongo wa mawazo kwa mhusika, pia viungo vya mwili kukosa uwezo wa kufanya kazi, kama inavyotakiwa.
Vilevile, anasema asilimia 25 ya wanawake walioko kwenye ndoa, wanakutwa na tatizo la ugumba, chanzo ikiwa ni utoaji mimba kabla, wakiwa wametumia njia zisizo salama kiafya.
Anarejea rekodi iliyoko ni kwamba, kinamama wengi wanapoteza maisha kwa kutotumia njia zisio sahihi, kwa sababu wanashindwa kupata huduma nzuri, pale wanapokuwa wanatoa mimba.
Hisia zao zinatajwa ni kwamba wanasita kufika hospitalini, wakihofu namna ya kujielezea, kabla ya kupatiwa huduma. Hilo nalo, linaingia katika hesabu ya kuwapo kundi la wanaopoteza maisha kwa kukosa huduma na wanaofika hospitalini, wakiwa wamechelewa kupatiwa huduma.
WAATHIRIKA WANENA
Binti mmoja wa umri miaka 24 (jina lake limehifadhiwa) kwa sasa mkazi wa Mbezi Luis, Dar es Salaam, anaelezea namna alivyopata shida baada ya kutumia dawa za kutoa mimba, ikamfanya ashindwe kufikia malengo aliyojiwekea shuleni.
“Nilinunua dawa kwa dada ambaye hakuwa hata na duka la dawa, bali alikuwa ana duka la nguo pamoja na urembo wa wanawake. Lakini cha kushangaza, dawa hizo alikuwa nazo na ilionekana kuwa huwa anawauzia wanawake wengi.
“Baada ya kupatiwa dawa zile, bila ya kujua mimba yangu ilikuwa na miezi mingapi kwa kipindi hicho, matokeo yake nilitokwa na damu nyingi sana, maumivu ya tumbo makali na nilitokwa na harufu mbaya ... takribani ya miezi mitatu,” anasimulia mhusika wa tukio hilo.
MAONO KISERA
Shirika la Afya Duniani (WHO), lilitoa mwongozo mpya kuhusu huduma ya utoaji mimba, lengo ni kulinda afya ya wanawake na wasichana, kuzuia wastani wa mikasa milioni 25 duniani vya utoaji mimba usio salama kila mwaka.
Kurejea utafiti wa kisayansi wa WHO, mwongozo husika ukaibua zaidi ya mapendekezo 50 yanayohusu huduma za kitabibu, utoaji huduma za afya na uingiliaji kati kisheria na kisera, kusaidia matukio ya utoaji mimba yaangukie katika usalama.
Hata hivyo, kuna mtazamo kwamba kutokuwapo elimu na uhamasishaji wa kutosha wa afya ya uzazi kwa makundi mbalimbali na hasa vijana na wanaume, kumesababisha kuenea mimba zisizotarajiwa na kuongezeka magonjwa ya ngono, hasa vijijini.
Pia, kunatajwa mila potofu zimechangia kuzorotesha afya ya uzazi katika baadhi ya maeneo.
SHERIA ILIVYO
Mwanasheria wa kujitegemea, Peter Majanjara, anaeleza namna utoaji mimba kwa wanawake wengi wanaotumia njia zisizo sahihi na sheria ya nchi haingalii mazingira halisi.
“Sheria haijaweka mazingira, kwa maana ya kwamba mtu amebakwa, amepata mimba kwa kujamiiana, basi anaweza kutoa mimba, sheria ya nchi hapo ipo kimya,.” anaeleza mwanasheria Majanjara.
Tamko la Sera ya Afya ya Mwaka 2007; serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakikisha “utoaji wa huduma bora za uzazi katika vituo vya kutoa huduma za afya zinazowavutia wanawake, wanaume na vijana.”
Aidha, kisheria, utoaji mimba ni kosa la jinai na ina adhabu kali, hata inatajwa kuchangia baadhi ya wanawake kutumia njia za mafichoni.
Kimsingi, ni adhabu inayoweza kumfunga mtu, kulingana na uzito wa kosa husika, kisheria ikiwaangukia mhusika mkuu na anayeshiriki kutoa mimba kinyume na sheria.
Mwanasheria Majanjara, anasema kwa sasa kuna jitihada zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa nafasi zao, kushinikiza kupungua matukio ya utoaji mimba kwa njia zisizo sahihi.
Anasema, ili kutumia njia sahihi za utoaji mimba, kunatakiwa kuwapo mtu mwenye uelewa kitaalamu, pia mamlaka sahihi inayohusika kitabibu katika namna ya kumsaidia mwanamke mjamzito.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED