GERTRUDE MONGELA; Afichua siri alivyofanikisha Beijing

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 05:53 PM Apr 24 2025
Mama Beijing Gertrude Mongela akiwa na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, hivi karibuni.
Picha: Mtandao
Mama Beijing Gertrude Mongela akiwa na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, hivi karibuni.

JINA ‘Gertrude’ asili yake ni Kijerumani, likimaanisha mkuki au fumo madhubuti, imara na lenye nguvu. Ndilo jina la Mwenyekiti na Mratibu wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) wa Wanawake wa Beijing, Balozi Gertrude Mongela.

Mama Beijing huyu, mwaka huu anatimiza miaka 80, baada ya kushuhudia miongo mitatu ya mkutano huo aliouandaa na kufanyika 1995, kuusimamia na hatua kwa hatua kufuatilia utekelezaji wake.

Hivi karibuni, anazungumza kwenye kongamano la kitaifa la maadhimisho ya miaka 30+ ya mafanikio ya Mkutano wa Beijing, linaloandaliwa na Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi likifanyika Dar es Salaam, akieleza siri ya kuufanikisha mkutano huo.

Anawamegea siri kuwa ni ‘kutunisha misuli’ kama jina lake alitumia ujasiri, na nguvu, akikataa kukutana na kuzungumza na viongozi ambao si wakuu wa nchi, badala yake akafanya mazungumzo kuhusu mkutano huo na vigogo wenye mamlaka na maamuzi ndani ya mataifa na serikali zao.

Akinguruma kwenye kongamano hilo la maadhimisho ya miaka 30+ ya mafanikio ya Beijing, anasema alikuwa jasiri na jeuri akapanga kuwa ni lazima vikao vya kuzungumzia mkutano huo viwe na viongozi wa juu kuanzia rais, makamu, waziri mkuu au hata wafalme kwa vile ndiyo wenye maamuzi na rasilimali na kuunga mkono.

Aidha, anawaambia, alizunguka karibu dunia nzima kuuzungumzia na aliokutana nao ni viongozi hao wakuu akiamini kuwa ajenda ya mwanamke si ya ‘katibu kata’. Ni ajenda ya juu zaidi ambayo lazima kutafuta wanaofanya maamuzi, wenye rasilimali na kupanga mipango ya kuyatekeleza si suala la kutafuta makubaliano.

Wakuu wa taasisi na masharika mbalimbali duniani ni miongoni mwa aliokutana nao, akimtaja Mkuu wa Kanisa Katoliki Dunia Papa Yohana Paulo wa II. Anasema alimfikia mahususi kujadili ajenda ya utoaji mimba na matumizi ya njia za uzazi wa mpango, ambayo alijua ingeibuka kwenye mkutano huo.

Kanisa Katoliki linapinga utoaji mimba na kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango hasa vidonge, sindano, vijiti na vitanzi.

Balozi Mongela anawaambia wanawake wanaharakati kuwa katika maandalizi walianza kukusanya taarifa kutoka ngazi za chini, kisha wilayani, taifa na hadi kiwango cha mabara, hivyo walipofika Beijing walikuwa na kila kitu yakiwamo mawazo ya wanawake wa ngazi za chini. Kisha wakakutana na wanawake ‘wazito’ kuandaa tamko la pamoja ndiyo maazimio 12 ya mkutano huo uliofanyika mwaka 1995, yanayoitwa Ulingo wa Beijing au Beijing ‘Platform of Action.”

Anasema kupata mapema taarifa za maoni ya wanawake kwenye ngazi za chini hadi mabara na kuzichambua ni moja ya mambo yaliyofanikisha jukwaa hilo.

Anawataja wanawake wa Tanzania kwa kusimama naye akisema alipoteuliwa na Katibu Mkuu wa UN Boutros Boutros-Ghali, alirudi nyumbani na kukutana nao wakimpa ushauri, nguvu na mbinu za kufanikisha mkutano huo, akisema wamekuwa pamoja muda wote wakifanyakazi kwa ushirikiano.

Akizungumzia harakati anakiri amezaliwa mpigania haki na kwamba mwaka 1955, akiwa mtoto Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, alifika Ukerewe kuitangaza TANU na harakati za uhuru, lakini bila kujali umri wake aliingia kwenye gari lililobeba wajumbe wa TANU kwenda kwenye mkutano na Mwalimu, akitoroka bila ruhusa, akashirikia mkutano akijificha asionekane.

“Nilikuwa nina kiherehere japo mtoto, lakini nilisikia habari za TANU na uhuru. Si hivyo tu hata nilipokuwa mtoto nilikuwa nauliza maswali kwa mama kama mbona baba hatusaidii kufanya jambo kwa mfano hata kuwasha moto…” anasema akiongeza kuwa alikuwa mtetezi na mwana harakati tangu mwanzo.

ANAIPA HAZINA KAZI

Mgeni rasmi wa kongamano hilo alikuwa Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, ambaye Mama Beijing alimpa jukumu la kurejea miradi ya ukandarasi inayotolewa na serikali akokotoe fedha zinazotolewa na Hazina iwapo zinawafikia wanawake?

“Mfano mtasema tumejenga hospitali nakubali, aliyeijenga ni nani, alipewa kandarasi na nani? Mwanamke ana nafasi kubwa katika maendeleo ya jamii. Tunao pesa zimeingia kwenye miradi mikubwa na zimeishia kwenye mikono ya wanaume, wanawake wamebakia kutazama.”

Anamweleza kuwa majengo makubwa ya makao makuu Dodoma yanajengwa, lakini ana wasiwasi hakuna mwanamama aliyepewa zabuni, akisema fedha zinatoka kwenye kodi za wanawake wakulima,  wakaanga vitumbua na zinaingia kwenye mfuko mkuu wa hazina, lakini baada ya kuweka kwenye bajeti zinekwenda taratibu kwa makandarasi wa kila aina wakiwamo Wachina, hivyo wanawake wanataka kufahamu ni pesa ngapi zimewafikia kwenye ujenzi huo?

“Tumekuwa na bajeti ya kilimo wanawake wanasifiwa sana wanavyolima tuambie zile fedha za miradi ya kilimo zimekwenda kwa wanawake wangapi? Shilingi ngapi zimekwenda kwa wanawake, wataalamu? Tunazungumzia kuongeza thamani ya mazao, ni pesa kiasi zinakwenda kwa mama anayelima mpunga na kikundi chake ili kuongeza thamani ya mazao yao?

Anakumbusha haifurahishi kuona pamba inachukuliwa inaongezwa thamani, wanawake wanabaki kununua kanga na vijora pekee kwa ajili ya sare.

Anazungumzia kufanyakazi za harakati zaidi, ili kuifanikisha Beijing wakianza na kuiangalia dira ya maendeleo 2025-50 kama imejumuisha masuala ya Beijing na kueleza ni lazima wanawake wahakikishe ina maono yao.

Anawataka kuiwahi ilani ya uchaguzi 2030 kufuatilia masuala ya usawa kijinsia na kuunganisha na utekelezaji wa Maazimio ya Beijing, akiwataka kutafsiri Azimio la Beijing na kulifikisha vijijini, Watanzania waambiwe kuhusu masuala ya Beijing, waone na wajue wajibu wao na wa serikali.

DUNIA KUMSHANGILIA

Mwaka huu Septemba inatimia miaka 30 baada ya Mkutano wa Beijing, naye atatimiza miaka 80, akisema wadau wake watafika kuserebuka pamoja naye Julai 31, Siku ya Mwanamke wa Afrika. “Wadau wa nje na ndani watakuja kusherehekea miaka 80, tutaanza Julai 31, Agosti 1, 2 hadi 3...”

Mama Mongela anakerwa na jembe la mkono, akisema: “Wanawake wasaidiwe kutumia teknolojia, kutumia jembe la mkono kukome, kupanda kwa mkono basi…wanawake wameumia, bibi aliumia, mama waliteseka walikunja migongo walichoka hata leo kizazi kinazidi kuchosha. Hapana jembe la mkono likome.”

Anasema siyo lazima liwe la mtu mmoja serikali na wadau watumie mbinu ya kuweka ‘senta za matrekita’ wanawake wachukue walime, wakivuna walipe. “Waziri Chande nakuomba. Teknolojia itumike kuwasaidia wanawake.”

“Wanawake wafundishwe masuala ya teknolojia kama ambavyo iliwekwa elimu ya watu wazima. Jioni wanawake wafundishwe TEHAMA, maadamu walifundishwa elimu ya watu wazima kusoma ABCD sasa TEHAMA ije,” anasema.

 KUJITEGEMEA

Anasisitiza kumkumbuka Mwalimu Nyerere, na falsafa ya ulazima wa kujitegemea na kuacha kupiga magoti kila mahali kuomba.

Anazungumzia uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani kuondoa misaada ya maendeleo kwa mataifa mengine na kuweka ushuru mkubwa kwa bidhaa zinazoingia Marekani kwa nchi nyingi duniani, akisema uwakumbushe Watanzania falsafa ya Nyerere ya kujitegemea.

“Amekataza dawa za malaria na UKIMWI zitoke Marekani. Namuona Nyerere akituaambia mjitegemee. Waafrika hatuna mjomba tujitegemee. Kila kitu kipo tunakwama wapi? Tusaidieni wanawake taifa letu kujitegemea. Kama wenzetu wanaume wameshindwa kufikiri tuwasaidie, wamekwama wapi?

 Anasisitiza kuwa kufikia hatua ya kujitegemea kunahitaji ushiriki wa kila mmoja, akitoa wito mahususi kwa wanawake wasibaki nyuma katika safari hiyo ya maendeleo.