NI safari ya wiki kadhaa kutimu miaka minne ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuwa madarakani katika awamu ya sita ya uongozi.
Eneo mojawapo anabaki na ‘umama’ wake, unasimama katika ustawi wa jamii, mahsusi katika maslahi yao, mama na mtoto.
Rais Dk. Samia, baada ya kuchukua uongozi wa nchi, akajikita katika mageuzi ya kina katika mageuzi ya kisera na kisheria, kutetea maslahi ya kundi hilo, chini ya wizara inayohusika na ustawi wa jamii.
Ufafanuzi wa wizara hiyo unagusa mageuzi katika sheria ya mtoto iliyoko, katika utaratibu wa kuasili watoto na malezi ya kambo.
Pia, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum, inataja katika Sera ya Wazee ya Mwaka 2003 toleo la 2024, inafanya maboresho ya miongozo na mikakati, ukiwamo Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji Makao ya Watoto 2023.
Kimsingi, ni wizara ambayo zao la ubunifu wake Rais Dk. Samia, akiwa na miezi 10 madarakani, kuwatetea hasa, kinamama na watoto, hadi kufikia sura pana ya jamii. Ameiunda mnamo Januari 2022, katika mtazamo kiserikali kwamba “kuleta ufanisi katika utoaji huduma za kijamii.”
Pia, yanatajwa maudhui mengine ni Uanzishwaji na Uendeshaji wa Mabaraza ya Ushauri ya Wazee, 2023; Mwongozo Kabambe wa Upangaji, Mipango na Taarifa za Ustawi wa Jamii ngazi ya halmashauri.
Pia katika jicho kuu la umma hiyo sasa na huko nyuma, inalenga kujikita katika Kusimamia Programu za Watoto Wanaoishi katika Mazingira Hatarishi, hata changamoto zao waliko mtaani.
KILICHOVUNWA HADI LEO
Ripoti ya kiserikali, ikiwamo kutoka wizara yenye kusimamia watoto, inafafanua katika utekelezaji wa sera na sheria, wizara hiyo ilichangia mabadiliko ya marekebisho ya Sheria ya Mtoto iliyoko sasa.
Hapo ni katika kipengele cha utaratibu wa kuasili watoto na malezi yake, yule wa kambo akatoa ushuhuda wa mavuno katika idadi ya waliopata malezi.
Kwa mujibu wa ripoti ya kiserikali, takwimu zilizoko za malezi kwa watoto wakambo, ikionyesha takwimu za waliopata malezi mwaka 2022 walikuwa 48 na wakafika 159 mwaka 2024.
Vilevile kwa walioasiliwa, ndani ya miaka hiyo ni; kutoka 56 mwaka 2022 hadi 133 mwaka 2024.
Maeneo mengine yanayotajwa ni malezi mbadala kwenye jumla ya watoto 2,017 wamehudumiwa; vilevile malezi ya kambo 1,803, ikilinganishwa na watoto 110 waliohudumiwa awali mwaka 2022.
“Ongezeko hilo limesaidia kupunguza uwapo wa watoto katika makao ya kulelea watoto wadogo nchini, pia imetoa fursa ya watoto walio katika mazingira hatarishi kulelewa katika familia.
“Katika kutatua changamoto ya ongezeko la watoto wa mitaani, Wizara imefanikiwa kuwatambua na kuhudumia watoto 23,601, wanaoishi na kufanya kazi mitaani, tofauti na watoto 3,957 kwa mwaka 2022,” inafafanua taarifa.
“Hii imeenda sambamba na kuanzishwa kwa Umoja wa Wamiliki wa Makao ya Watoto nchini, ili kuimarisha usimamizi pamoja na usajili,” anafafanua.
Mengine yanayotajwa kuanzishwa, yanajumuisha Mwongozo wa Taifa wa Uendeshaji, Usimamizi na Uratibu wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Migogoro ya Ndoa, 2023.
Kabla ya hapo mwaka 2022, vilibuniwa Kiongozi cha Kanuni za Maadili ya Kufanya Kazi na Watoto; na Kiongozi cha Mlezi wa Watoto.
Ndani ya mwaka huo, pia kuna Mwongozo wa Mafunzo ya Uwiano wa Kijinsia na Ujumuishaji wa Jamii.
Sasa infafanuliwa kwamba, ni mageuzi ya ongezeko lililosaidia kupunguza uwapo wa watoto katika makao ya kulea watoto wadogo.
WATOTO, MAKAO YAO
Sasa inatajwa kwamba, kuanzishwa kwa Umoja wa Wamiliki wa Makao ya Watoto nchini kumelenga kuimarisha usimamizi pamoja na usajili wake.
Kwa ujumla, serikali inatajwa kuongeza makao makuu ya watoto kufika 374 hadi kufika mwaka jana, kutoka 224 wakati inasajiliwa.
“Makao ya watoto hutoa makazi ya muda kwa watoto walio katika mazingira hatarishi, wakiwamo watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani,” anasema.
Taarifa ya kiserikali inafafanua kwamba, katika kuendelea kumpa fursa za kiuchumi mwanamke na familia yake imeimarisha mifumo ya malezi ya watoto wadogo mchana na kijamii.
PICHA YA TAKWIMU
Inatajwa kupitia takwimu zake kwamba, katika miaka minne hadi sasa, usajili wa vituo vya kulea watoto vimeongezeka kutoka 1,543 mwaka 2022 hadi 3,862 mwaka jana na kijumla kitaifa kuna uwezo wa kuhudumia watoto 397,935.
“Uwapo wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana na vya kijamii umetoa fursa kwa wazazi/walezi kushiriki katika shughuli za kuingiza kipato kwa amani, wakati watoto wakiwa katika uangalizi salama,” yanafafanua maelezo husika.
USALAMA WAO
Kuna eneo lingine la mageuzi yaliyoshikamana na teknolojia mtandao, katika zama za miaka minne anayowajibikia. Ni kwa Rais Dk. Samia, kuzindua Kampeni ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni.
Ni hatua inayotajwa kuendana na kuwapo jumla ya shule 679 za msingi na 109 na za sekondari katika mikoa 16 ilikofikiwa.
Manufaa yake yanatajwa na serikali kwamba, kuwapo jumla ya watoto 821,593, kutoka shule za msingi 735,991.
Vilevile inatajwa, kuwapo shule za sekondari 85,602 na walimu wao 3,909 waliopatiwa usalama wa mtoto mtandaoni.
Eneo hilo linataja kuwapo jumla ya vijarida 112,517 na vipeperushi 2,000 vilivyosambazwa kunufaisha usalama wa mtoto aliko, kupitia nyenzo mtandao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED