NI simulizi zenye fursa chanya kitaifa, pale ukanda wake wa kimazingira, unajibu katika tafsiri ya rasilimali uchumi.
Katika lugha nyepesi ni kwamba, mazingira ya kitaifa ikipewa ubatizo wa ukanda, sasa unabeba ujumbe “mazingira yanaweza kupumua rasilimali mafuta na gesi.”
Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), inasema ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa kuendesha mnada wa duru ya tano ya kunadi vitalu 26 vya gesi asilia na mafuta kitaifa.
Ni aina ya mchakato huo wa kuendesha mnada kunadi vitalu kwa ajili ya kuwakaribisha wawekezaji katika sekta hiyo ya uzalishaji wa gesi asilia nchini.
Ni maudhui yatokanayo na mafunzo maalum kwa wanahabari jijini Dar es Salaam hivi karibuni, yaliyoandaliwa na mamlaka hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Shigela Malosha, anasema kati ya vitalu hivyo 26 vitakavyonadiwa, 23 vinapatikana katika Bahari ya Hindi na vitatu Ziwa Tanganyika.
Malosha anasema, maandalizi kwa ajili ya kazi hiyo tayari yamekamilika na kinachosubiriwa ni kuidhinishwa nyaraka moja, ambayo serikali iko katika hatua ya mwisho, baada ya hapo mnada wa vitalu utazinduliwa.
Malosha anasema, mwekezaji mwenye mtaji na teknolojia sahihi ya utafutaji na uzalishaji mafuta na gesi asilia, atapatiwa nafasi ya kuwekeza, kwa sababu lengo kubwa ni kuhakikisha sekta hiyo inachangia kwa kiwango kikubwa kwenye pato la taifa.
“Mpango wa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuweka nguvu zaidi katika suala la utafutaji wa mafuta na gesi, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inahamasisha nishati safi ya kupikia.
”Mchango wa sekta ya gesi asilia kwa taifa ni mkubwa sana, kwa sababu tangu tumeanza uzalishaji wake mwaka 2004 umekuwa na manufaa makubwa sana.
“Matumizi yote ambayo yamekuwa yakitokana na uzalishaji wa gesi asilia, unakwenda kutumika pia kwenye viwanda, hotelini, kwenye magari, na majumbani kwa mtu mmoja mmoja,” anafafanua.
Mbali na vitalu hivyo 26 vinavyosubiri mnada, pia anasema kuna vitalu ambavyo vimeshafanyiwa utafutaji na sasa viko katika hatua ya kuhakikiwa.
Anavitaja vitalu hivyo Ruvu na Mkuranga mkoani Pwani na kwamba tayari vilishafanyiwa utafutaji na ugunduzi vinasubiri kuhakikiwa.
“Lakini ili uende katika hatua ya uendelezaji lazima uhakiki. Kwa hiyo, kampuni ziko katika hatua za kuhakiki, ili kuona kwamba je ugunduzi huo unaweza kuwa mradi wa kuendelezwa,” anasema Malosha.
VILIKO VITALU VIPYA
Malosha anaeleza zaidi kuhusu vitalu 26 vinavyosubiri mnada, kwamba vinapatikana katika maeneo mawili, 23 viko katika mkondo wa bahari na vitatu viko mkondo wa Ziwa Tanganyika.
“Vitalu hivi vimeshabainishwa na tayari data na taarifa zake zimeshaandaliwa, pia nyaraka za zabuni zote zimeshaandaliwa kwa maandalizi yote.
” Kwa kifupi, maandalizi yote yameshakamilika na sasa hivi kuna nyaraka moja ambayo ni mkataba wa kifani wa kugawana uzalishaji na mapato, ambao serikali iko katika hatua za mwisho kuuidhinisha.
“Mkataba huu unaosubiriwa, utakuwa sehemu ya nyaraka hiyo ya zabuni ambayo ataitumia pia mwekezaji kwa ajili ya kuangalia masharti na vigezo ili kuingia mkataba au kama atakuwa ameshindwa kwa kutumia vigezo na masharti ambayo yamewekwa kwenye mktaba huo kifani,” anaeleza bosi huyo.
Anaendelea: “Waje wachangamkie fursa pale tutakapofanya mnada, waitumie kwa ajili ya kuchukua kitalu chochote kulingana na sifa atakazokuwa nazo huyo mwekezaji.”
Kwa mujibu wa Malosha, kupatikana wawekezaji, kutaongeza uzalishaji wa gesi asilia pamoja na mafuta nchini.
“Nasema tutaongeza uzalishaji kwa sababu tayari tulishagundua. Kwa hiyo, tukipata hao wawekezaji, tutaendelea kutafuta na tutaongeza ugunduzi pamoja na uzalishaji wake.
“Cha pili, kwa jamii husika wawekezaji hao ambao watapatikana katika maeneo mbalimbali ambayo tumeyabainisha, nao watanufaika katika namna tofauti, ikiwamo kutoa kuhduma za chakula, afya, barabara na nyinginezo.
“Kwa hiyo, itakuwa na manufaa kwa nchi lakini na kwa mwananchi mmoja mmoja,” anasema Malosha.
ILIKOTOKA MIRADI GESI
Kwa mujibu wa PURA, tangu kuanza uzalishaji wa gesi asilia nchini mwaka 2004 hadi Januari mwaka jana, kiasi kilichotumika ni futi za ujazo bilioni 700 kati ya trilioni 57 zilizogundulika. (asilimia1.23)
Tanzania imegundua kiwango kikubwa cha gesi asilia katika ukanda wa pwani ya Lindi na Mtwara, rasilimali ambayo inajulikana kama “gesi ya kina kirefu cha bahari” kwa kuwa inapatikana zaidi ya kilomita 100 kutoka pwani kwenye kina cha maji hadi kilomita 2.5.
Kutokana na kiasi hiki cha gesi kilichogunduliwa, Tanzania inatajwa itaweza kuitumia kwa miaka mingi kulingana na viwango vya sasa vya matumizi, kama kuzalisha umeme.
Kadhalika, upanuzi wa matumizi ya gesi kama viwandani, pia nchi jirani inaelezwa itaifanya Tanzania kuwa kitivo cha nishati ya gesi katika ukanda huu wa nchi za Africa Mashariki.
Pia, kuna ufafanuzi kwambaTanzania iko katika mchakato wa kutekeleza Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG), ambao baada ya kukamilika utakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi.
Ni dira inayotoa ajira zaidi 1,000 sehemu kubwa ya gesi asilia iliyogunduliwa nchini hadi sasa iko baharini kwenye kina kirefu.
LNG ni gesi asilia iliyopoozwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa hadi kufikia kiwango cha nyuzi joto -161 kuwa rahisi kubeba na kusafirisha.
Hata hivyo, inatajwa katika mradi wa LNG serikali imeamua mtambo wa uchakataji gesi utajengwa na kuwekwa nchi kavu na sio baharini.
Faida nyingine za kiuchumi inatajwa kuwa pamoja na kuiwezesha serikali kuendeleza sekta ya umeme na viwanda, ikiwa ni pamoja na kufanikisha uanzishwaji ukanda wa viwanda (Industrial Park) kwa ajili ya uwekezaji katika viwanda vya kemikali saruji, na mbolea.
Lengo kuu la mradi wa LNG ni kuuza na kusafirisha gesi nje ya Tanzania.
TPDC NA GESI
Wakati haipo wazi au rasmi hali ya uzalishaji mafuta nchini kuonekana hatua ya ngazi ya soko, kama ilivyo kwa gesi, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) lina matamshi yake kuhusu gesi, bidhaa inayohusika nayo pia kuisambaza sokoni.
Kupitia tamko kwenye kikao chake cha wafanyakazi, mnamo Februari 18 mwaka huu mjini Morogoro, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue, ananukuliwa na tovuti yake kuhusu hatua kadhaa za kunadi gesi.
Hapo inagusa mpango mkakati, ikiwamo kuongeza kiwango cha upatikanaji gesi na kuongeza kasi ya usambazaji wake, kwaajili ya matumizi mbalimbali.
ILIKOTOKA GESI
Kurejea tovuti ya Manispaa ya Songea, Septemba 2018, gesi asilia iligundulika kwa mara ya kwanza nchini mwaka 1974 katika kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi.
Pia, ikawa mkoani Mtwara mwaka 1982, eneo la Mnazibay, gesi asilia iliyogundulika nchi kavu na baharini ikifikia takriban futi za ujazo trilioni 55.08, zikiwa ni takwimu hadi kufikia Machi 2015.
Tovuti hiyo, inamnukuu Mhandisi Mwandamizi kutoka TPDC, Mhandisi Modestus Lumato, aliyezitaja changamoto za sekta ya mafuta na gesi inajumuisha gharama kubwa kwa wakati huo, ikakadiriwa uchimbaji kisima cha utafiti kugharimu Sh. bilioni160.
Pia, ikatajwa gesi asilia inaweza kupatikana katika miamba tabaka (sedimentary rocks), Tanzania kukitajwa maeneo pwani Mtwara na Lindi na mabonde ya nchi kavu.
Hatimaye uzalishaji ukaaanza mwaka 2004, huku ukibeba ufafanuzi wa kiuzalishaji kuvunwa
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED