Wizara ya Mifugo na Uvuvi imezindua rasmi zoezi la kulinda mazalia na makulia ya samaki katika Ziwa Victoria kwa kuweka maboya 32 katika mipaka ya maeneo maalumu yaliyotengwa, ambapo shughuli za uvuvi hazitaruhusiwa kufanyika.
Zoezi hilo limezinduliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Edwin Mhede, katika mwalo wa Shadi uliopo ndani ya Ziwa Victoria. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dk. Mhede amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kudhibiti uvuvi haramu, hasa katika maeneo nyeti ya uzalishaji wa samaki.
“Serikali imeamua kuchukua hatua hii ili kulinda rasilimali za uvuvi kwa kuhakikisha kuwa maeneo maalumu ya mazalia na makulia ya samaki yanahifadhiwa ipasavyo, bila kuingiliwa na shughuli za uvuvi zisizoruhusiwa,” amesema Dk. Mhede.
Ameongeza kuwa uwekaji wa alama maalumu katika maeneo hayo ni hitaji la kikanuni, likilenga kutambua na kulinda maeneo muhimu kwa ajili ya kuendeleza uvuvi endelevu. Alibainisha kuwa maeneo hayo yamebainishwa kwa ushirikiano kati ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya uvuvi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED