Wanawake waaswa kuchangamkia mikopo ya asilimia 10

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 03:59 PM May 21 2025
Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Rehema Sanga.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Rehema Sanga.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Rehema Sanga, amewahimiza wanawake kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ili kujikwamua kiuchumi na kuepuka kuingia katika mikopo kandamizi inayojulikana kama “mikopo ya kausha damu”.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe Digital jijini Dar es Salaam, Rehema ameeleza kuwa lengo la jukwaa analoliongoza ni kuwawezesha wanawake kupata uelewa, maandalizi na stadi za msingi ili kufanikisha upatikanaji wa mikopo hiyo yenye masharti nafuu.

Changamoto Zinazowakabili Wanawake

Rehema ametaja baadhi ya changamoto zinazowakwamisha wanawake wengi kufikia mikopo hiyo kuwa ni pamoja na kutofahamu namna ya kujisajili katika mifumo rasmi ya serikali, pamoja na uelewa mdogo wa matumizi ya teknolojia kama vile kompyuta na simu za kisasa.

"Kutokana na changamoto hizi, jukwaa letu limejipanga kuendelea kutoa elimu ya namna ya kujiunga kwenye mifumo, kuunda vikundi vya pamoja, na kuandaa maandiko ya biashara yatakayowasaidia wanawake kupata mikopo kwa ufanisi zaidi," amesema Rehema.

Ushauri kwa Wanawake Wajasiriamali

Rehema amewasisitiza wanawake kuwa na maandiko ya biashara binafsi wanayokusudia kufanya badala ya kulazimisha kuingia katika miradi ya pamoja ambayo haiwezi kusimamiwa ipasavyo.

“Tunashauri mikopo hii itumike kukuza biashara zilizopo badala ya kuanzisha biashara mpya ambazo hazijafanyiwa utafiti wa kutosha. Kama mtu tayari ana duka, genge au biashara yoyote inayoendelea, huo ndio wakati muafaka wa kuomba mkopo kwa ajili ya kukuza,” amefafanua.

Aidha, amehimiza wanawake kujiunga katika vikundi vinavyoaminika, ambavyo vitatumika kama dhamana ya mkopo kwa wanachama wake. Kila kikundi kinapaswa kuwa na akaunti ya benki inayotumika kuweka akiba, jambo litakalorahisisha upatikanaji wa mikopo kutoka halmashauri.

Mikakati ya Elimu na Ushirikiano

Rehema amesema kuwa jukwaa litaendelea kutoa elimu kwa wanawake juu ya faida ya mikopo ya asilimia 10, namna ya kukuza mitaji na kutumia teknolojia kama simu za mkononi na kompyuta kusimamia biashara zao.

"Tunashirikiana na taasisi za kifedha kutoa elimu ya fedha, lengo likiwa ni kuwasaidia wanawake kutofautisha kati ya fedha zao binafsi na fedha za biashara ili kuimarisha uthabiti wa mitaji yao," ameongeza.

Shukrani kwa Viongozi

Katika hatua nyingine, Rehema ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuiwezesha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuwa miongoni mwa halmashauri 10 zilizonufaika na mpango wa mikopo hiyo.

Pia amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogoro, kwa kuwa mlezi wa jukwaa hilo na kusaidia kwa hali na mali kuhakikisha wanawake wanapata msaada wanaouhitaji.