Wananchi Kata ya Haubi wapambana na kilimo cha Bangi

By Zanura Mollel , Nipashe
Published at 04:43 PM May 21 2025
 Wananchi Kata ya Haubi wapambana na kilimo cha Bangi
Picha: Mpigapicha Wetu
Wananchi Kata ya Haubi wapambana na kilimo cha Bangi

Wananchi wa Kata ya Haubi, wilayani Kondoa mkoani Dodoma, wameamua kwa pamoja kukabiliana na kilimo haramu cha bangi ambacho kwa muda mrefu kimekuwa changamoto katika eneo hilo.

"Zamani bangi ilikuwa kama sehemu ya maisha yetu, lakini sasa tunaelewa madhara yake kiafya na kijamii," alisema Rajabu Hamis, mkazi wa Kijiji cha Mafai.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mafai, Shaibu Hamis Kalinga, amesema kuwa uongozi wa kijiji umejipanga vyema kuhakikisha wanatokomeza kabisa kilimo cha bangi kwa kutoa elimu ya madhara yake na kuhamasisha kilimo halali chenye tija.

“Tumeanzisha kampeni ya kutoa elimu kupitia mikutano ya kijiji, tunawashauri wakulima kuachana na bangi na kujikita katika kilimo cha mazao halali kama mahindi, alizeti na mbaazi,” ameeleza Kalinga.

Mafanikio ya Ushirikiano na Elimu kwa Umma

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kondoa, imefanikiwa kuteketeza jumla ya ekari 157 za mashamba ya bangi wilayani humo.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa DCEA, Daniel Kasokola, mmoja wa maofisa wa mamlaka hiyo alisema kuwa kupungua kwa idadi ya mashamba yaliyobainika mwaka huu ni kiashiria cha mafanikio ya jitihada za pamoja kati ya mamlaka na wananchi.

“Ushirikiano kutoka kwa wananchi umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza kilimo haramu. Hii inaonesha mafanikio ya kampeni ya elimu kwa umma na ushirikishwaji wa jamii katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya,” amesema Kasokola.

Wito kwa Jamii

DCEA imetoa wito kwa wananchi wa maeneo mengine nchini kuiga mfano wa Kata ya Haubi kwa kutoa taarifa za maeneo yanayojihusisha na kilimo au biashara ya dawa za kulevya, huku ikiendelea kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa kuhakikisha jamii inalindwa dhidi ya madhara ya dawa hizo.