BRELA yawageukia wasanii usajili wa ubunifu

By Restuta James , Nipashe
Published at 03:58 PM May 21 2025
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa
Picha: Mpigapicha Wetu
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa

Serikali imeelekeza nguvu zaidi kuwaelimisha wanamuziki umuhimu wa kusajili na kulinda kazi kisheria, ili waweze kunufaika na sanaa hiyo kwa miaka mingi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa, ameyasema hayo Dar es Salaam leo Mei 21, 2025, kwenye maadhimisho ya siku ya miliki ubunifu iliyoambatana na utoaji wa tuzo za tasnia hiyo kwa wasanii na wavumbuzi.

Amesema muziki ni biashara yenye thamani kubwa inayoweza kumnufaisha msanii na vizazi vyake kwa muda mrefu, kama utalindwa kisheria na kuepusha wizi wa ubunifu.

Nyaisa amesema licha ya muziki wa Tanzania kuvuka mipaka ya nchi, wasanii wengi bado hawajachukua hatua ya kusajili kazi zao, jambo linalowanyima fursa ya kunufaika na kazi hizo kisheria.

“Tunasisitiza muziki si burudani tu, ni biashara. Na biashara yoyote inalindwa. Wasanii wengi wanapoteza mapato kwa sababu kazi zao hazijasajiliwa,” amesema.

Amekumbusha kuwa haki ya ubunifu wa muziki ikiwamo sauti na mdundo, inaweza kulindwa kisheria kwa kusajili BRELA.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Jafo.
“Wapo wasanii wa zamani ambao nyimbo zao bado zinapigwa hadi leo, lakini hawapati chochote kwa sababu hawakuzisajili. Hili ni pigo kwao na kwa familia zao,” amesema.

Ameongeza kuwa mabadiliko ya teknolojia yamefungua fursa kwa wasanii na yameongeza changamoto ya matumizi holela ya kazi za muziki bila ridhaa ya wasanii.

Amesema wakala huo utaendelea kushirikiana na taasisi za serikali, ili kuhakikisha kazi za ubunifu zinalindwa na zinakuwa chanzo thabiti cha kipato na uchumi wa nchi.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Jafo, amesema moja ya mikakati ya serikali kuimarisha ubunifu na uvumbuzi ni kuandika Sera ya Taifa ya Miliki Bunifu, akiitaja kuwa dira muhimu ya kuendeleza ubunifu nchini.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Muziki na Miliki Bunifu Tanzania: Sikiliza Mdundo wa Miliki Bunifu.”