Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Tanzania Bara, Benson Kigaila, amesema kuwa Mei 21, 2025, itasalia kuwa siku ya kihistoria kwa kile alichokiita “kufungwa rasmi kwa ukurasa wa CHADEMA,” kufuatia viongozi na wanachama kadhaa kuhamia rasmi katika chama chake.
Akizungumza na Nipashe Digital, Kigaila amesema kuwa tayari CHAUMMA kipo katika maandalizi ya kuwapokea viongozi wapya waliotangaza kujiunga na chama hicho, na kueleza kuwa hatua hiyo ni mwanzo mpya wa mageuzi ya kweli ya kisiasa nchini.
“Chama kinapopoteza mwelekeo na malengo yake ya kuanzishwa, wanachama wanaoelewa huchukua hatua. Mimi mwenyewe niliwekeza nguvu nyingi kukipigania CHADEMA usiku na mchana, lakini badala ya kuthaminiwa, tumekuwa tukitukanwa na kudharauliwa. Kwa hali hiyo, ni wazi hatukuwa na sababu ya kuendelea kubaki. Tumeamua kujiunga na CHAUMMA, na tutahakikisha kinakuwa chama kikuu cha siasa nchini,” amesema Kigaila.
Ameeleza kuwa msingi mkuu wa chama cha siasa ni kushika dola kupitia mchakato wa uchaguzi, na kwamba kushindwa kushiriki uchaguzi ni sawa na kupoteza dira ya kisiasa.
Kwa mujibu wa Kigaila, uamuzi wa viongozi hao kuhama kutoka CHADEMA unaashiria mwamko mpya na kukubalika kwa ajenda ya CHAUMMA katika kuleta mabadiliko ya kweli kwa Watanzania.
Amesisitiza kuwa baada ya kupokea viongozi hao waandamizi, chama hicho kitaendelea na ziara katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha uenezi na kuvutia wanachama wapya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED