HIVI karibuni safu ya gazeti hili, ilikuwa na makala kuhusu utetezi kiafya kwa watoto waliozaliwa njiti (kabla ya umri wa kuzaliwa) na kwa upekee, nafasi ya taasisi ya kijamii Doris Fundation iliyojitolea. Nini ustawi wao kimaisha na kiuchumi? Nipashe imemdadisi mwanzilishi wa taasisi hiyo. Fuatilia....
DORIS Mollel, ni mwanamama amedumu katika kutetea haki za watoto njiti, akiwa mwanzilishi wa Asasi ya Doris Mollel Foundation (DMF), akiendelea kuleta mabadiliko makubwa katika ustawi wa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.
Kupitia juhudi zake na wadau wa msimamo wake, serikali hatimaye imepitisha sheria inayoruhusu likizo ya miezi minne kwa wanawake wanaojifungua watoto njiti, hatua inayolenga kusaidia malezi na uangalizi wa watoto hao. Doris, mwenye historia ya kuzaliwa njiti, ameshirikiana na serikali, wabunge, vyama vya wafanyakazi na wadau wa afya, kushinikiza mabadiliko hayo kitaifa.
Nipashe katika mazungumzo naye, anaeleza kwa kina safari yake kuhakikisha wazazi wa watoto njiti, wanaopata msaada kifamilia, kiafya na kijamii.
Hatua hiyo kihistoria, ni sehemu ya mapambano ya muda mrefu kuhakikisha watoto njiti wanapata huduma stahiki na kupunguza vifo vya watoto wachanga nchini. Endelea na mazungumzo:
SWALI: Nini kilikusukuma, hata ukawa mtetezi wa maslahi ya watoto njiti?
JIBU: Nilizaliwa kabla ya wakati, nikiwa na uzito wa gramu 900, huku pacha wangu akiwa na kilo 1.2. Mama yangu, aliyekuwa muuguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikumbana na changamoto kubwa ya kupangiwa zamu za usiku, wakati bado tulihitaji uangalizi maalum.
Aliteseka sana, akiomba asipangiwe zamu hizo. Hali hii ilinipa msukumo mkubwa wa kupigania haki za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na wazazi wao.
Zaidi ya hayo, nilipojifunza kuwa kuzaliwa kabla ya wakati kunachangia hadi asilimia 48 ya vifo vya watoto wachanga, niliona haja ya kuchukua hatua kupunguza tatizo hili.
SWALI: Kwa lugha nyepesi, mtoto njiti ni nani?
JIBU: Mtoto njiti ni mtoto anayezaliwa kabla ya wiki 37 za ujauzito. Changamoto zao zinafanana na watoto wanaozaliwa na uzito pungufu, hivyo wanahitaji uangalizi wa hali ya juu.
SWALI: Ulianzaje safari yako ya kuwa mtetezi wa haki za watoto njiti?
JIBU: Safari yangu ilianza kwa kutafiti changamoto zinazowakabili watoto hawa na wazazi wao. Baada ya kugundua kuwa hakuna sheria iliyokuwa inatambua likizo maalum kwa wazazi wa watoto njiti, niliamua kushirikiana na wadau mbalimbali kuanzisha mchakato wa kisheria wa kutetea haki hiyo.
Tulifanya mikutano ya kwanza mwaka 2017 na baadaye vikao vikaanza rasmi mwaka 2018, hadi tulipofanikiwa kushawishi serikali kufanya maboresho katika sera za likizo ya uzazi.
SWALI: Ni wadau gani mnashirikiana nao?
JIBU: Tunafanya kazi kwa karibu na serikali, kupitia wizara mbalimbali, ikiwamo Wizara ya Kazi, Wizara ya Afya, na TAMISEMI.
Pia, tunashirikiana na vyama vya wafanyakazi kama TUCTA, TUGHE na ATE, pamoja na vikundi vya wanawake kama Tanzania Women Parliamentary Group (TWPG) na Mtandao wa Wazazi wenye Watoto Njiti (Preterm Family Network).
Mashirika kama Women Fund Tanzania na Asas Diaries yamekuwa yakituunga mkono kwa hali na mali. Viongozi wanawake kama Mama Getrude Mongella (aliyeongoza kikao cha kinamama Beijing, mwaka 1995), Mama Anna Abdallah na Mama Zakia Meghji (wote mawaziri wastaafu), walihusika kwa kiasi kikubwa katika mchakato huu.
SWALI: Ushirikiano wenu na serikali ukoje?
JIBU: Ushirikiano wetu ni wa karibu sana, hasa katika utekelezaji wa miradi ya afya. Wizara ya Afya ni mshirika wetu mkuu, na TAMISEMI, inatusaidia kufanikisha shughuli zetu katika ngazi za jamii.
SWALI: Vipi kuhusu ushirikiano wa kimataifa?
JIBU: Tunafanya kazi kwa karibu na mashirika ya kimataifa kama WHO (Shirika la Afya Duniani ya Umoja wa Mataifa), ambayo yamesaidia kuimarisha juhudi zetu za kupambana na changamoto za watoto njiti.
SWALI: Mnafadhiliwaje kifedha?
JIBU: Vyanzo vyetu vya fedha vinatoka kwa wafadhili wa ndani na nje ya nchi, kupitia misaada ya kibiashara na michango ya hiari.
Pia tunafanya ‘Harambee’ (uchangiaji fedha) kwa ajili ya kununua vifaa tiba kwa watoto njiti.
SWALI: Ofisi zenu ziko wapi na mna wafanyakazi wangapi?
JIBU: Ofisi zetu kuu zipo Msasani, Oysterbay, Dar es Salaam na tuna wafanyakazi 11 wanaosimamia shughuli zetu kote nchini.
SWALI: Ni wataalamu gani mnashirikiana nao?
JIBU: Timu yetu inajumuisha wauguzi, wasimamizi wa miradi na wataalamu wa masuala ya kijamii, ambao wanafahamu changamoto za malezi na makuzi ya watoto njiti.
SWALI: Mnashirikiana vipi na watu wazima waliokuwa watoto njiti?
JIBU: Tumeunda mtandao wa wazazi wa watoto njiti, ambao ulianza na wazazi 10 na sasa una zaidi ya 270. Wanasaidiana kwa kushirikiana kupitia vikundi vya ‘WhatsApp’ (aina ya mtandao) na majukwaa mengine ya kijamii.
SWALI: Mnashirikianaje na sekta ya umma na binafsi (PPP)?
JIBU: Kazi zetu nyingi zinafanikishwa kupitia mashirika binafsi, yanayosaidia jamii kwa kutoa fedha na mahitaji mbalimbali kupitia CSR (Corporate Social Responsibility- Mfumo wa kitaasisi kuwajibikia jamii).
SWALI: Unahusishaje maisha yako binafsi katika harakati hizi?
JIBU: Mbali na kazi yangu, nimepewa jukumu la kusaidia uanzilishwaji wa Shule ya Jerusalem chini ya kanisa, jambo linalonipa fursa kutumia ujuzi wangu kusaidia jamii.
SWALI: Mnashirikiana vipi na wazazi wa watoto njiti?
JIBU: Tunazungumza nao mara kwa mara, kupitia vikundi vya mtandaoni na mikutano ya ana kwa ana. Wanashirikiana kusaidiana, pia kuibua changamoto zinazowakabili wengine.
SWALI: Hali ya watoto njiti nchini inaelekea kuboreka au kuwa mbaya zaidi?
JIBU: Kuna ongezeko la watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, linalochangiwa na mabadiliko ya tabianchi, afya ya wazazi, na hali ya maisha kwa ujumla. Tunatumaini maendeleo ya teknolojia yatasaidia kupunguza changamoto hizi.
SWALI: Nini ujumbe wako kuhusu watoto njiti na ustawi wao?
JIBU: Kila mtu anapaswa kutambua kuwa suala la watoto njiti si la Doris Mollel Foundation pekee. Watoto hawa wanazaliwa kila mahali na hali hii inaweza kumkuta mtu yeyote, awe na uwezo wa kifedha au la. Kila mmoja wetu ana jukumu la kusaidia kuboresha ustawi wao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED