Nne-bora Ligi Kuu ilivyo vita ya jasho na damu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:10 AM Mar 03 2025
Mchezaji wa Azam FC, Feisal Salum
Picha: Mtandao
Mchezaji wa Azam FC, Feisal Salum

LIGI Kuu Tanzania Bara inaelekea ukingoni ikibakisha raundi nane tu ili iweze kutamatika kwa msimu wa 2024/25. Mbio za ubingwa zimekuwa za kukata na shoka, ambapo msimu huu Simba na Yanga hazijaachana mbali kama misimu kadhaa iliyopita.

Kwa kipindi kama hiki, timu hizo zinakuwa zimeshaanza kuachana pointi tano mpaka saba kwa michezo sawa, lakini safari hii zinaachana pointi moja, au mbili hivi.

Kutokana na mbio hizi za mafahari wawili ina maana atakayeshindwa kutwaa ubingwa ataangukia kwenye nafasi ya pili.

Kwa maana hiyo timu zilizobaki msimu huu inaonekana ni ngumu sana kupata nafasi ya pili kama ambavyo ilivyokuwa msimu uliopita, ambapo hakukuwa na mbio za kuwania ubingwa, bali Yanga ilijijengea kijiji chake, huku Simba na Azam ndizo zilizokuwa zikiwania nafasi ya pili, na hatimaye kuangukia kwa 'Wanalambalamba' hao.

Msimu huu ukiondoa farasi hao wawili kwenye mbio za ubingwa, shughuli pevu ya jasho na damu ipo pia katika kuwania nasi ya tatu na ya nne, ambapo kumeonekana kuna upinzani mkali kati ya Azam FC, Singida Black Stars na Tabora United.

Kwa jinsi msimamo ulivyo ni kwamba kuna asilimia kubwa kati ya timu hizi tatu, mbili kumaliza nafasi hizo na moja ikatupwa nje.

Ikumbukwe kuwa timu itakayomaliza nafasi ya tatu moja kwa moja inapata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, huku ya nne ikipata nafasi kama hiyo, kama bingwa wa Kombe la FA itakuwa miongoni mwa timu mbili zitakazomaliza nafasi za juu kwenye Ligi Kuu.

Katika makala haya tunakuchambulia timu zinazowania kumaliza nafasi ya tatu na nne, huku zikionekana hazina uwezo wa kwenda kuzisumbua Simba na Yanga kwenye nafasi mbili za juu ya msimamo wa ligi

1# Azam FC

Inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na pointi 45, ikicheza michezo 22 na kusalia na michezo minane. Imezidiwa pointi tisa na Simba, iliyo juu yake kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa ligi.

Ingawa kwenye mpira lolote linaweza kutokea, lakini inaonekana ni ngumu mno kwa Azam kuota ubingwa au nafasi ya pili kwa sasa, zaidi ya hiyo iliyonayo au ya nne.

Siyo hivyo tu, kama ikifanya vibaya inaweza kukosa hata nafasi ya nne, kwani msimu huu kuna timu tatu ambazo zinawania nafasi hizo mbili.

Kutokuwa na rekodi ya kutopoteza mechi kirahisi, au kupata sare kwa nadra kwa timu za Simba na Yanga, kunaifanya Azam kuwa kwenye wakati mgumu kuwafikia huko juu.

Yanga imecheza michezo 13 bila kupoteza, ikipata sare moja tu, tangu ilipofungwa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United, Novemba 7, mwaka jana, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Simba tangu ilipopoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga, Oktoba 19, mwaka jana, imecheza michezo 15 bila kupoteza, ikiwa ndiyo mechi pekee kupoteza mpaka sasa msimu huu.

Hii ni tofauti na Azam, ambayo imetoka kupata sare michezo yake miwili mfululizo ya mabao 2-2 dhidi ya Simba na 1-1 dhidi ya Namungo, Februari 9, mwaka huu, ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Pamba Jiji FC.

Kukosekana kwa mfululizo wa ushindi ndiyo unaowaondoa Azam kwenye ubingwa na ushindi wa pili, huku ikitakiwa kufanya kazi ya ziada msimu huu kupata nafasi ya tatu na nne, kutokana na ushindani mkubwa kuongezeka.

2# Singida Black Stars

Ni timu iliyosheheni nyota ambao wengi wao walikuwa wanahitajika kusajiliwa na Klabu za Simba na Yanga.

Wachezaji hao ni kama beki raia wa Ivory Coast, Antony Trabita, straika raia wa Ghana Jonathan Sowah aliyesajiliwa dirisha dogo la usajili na winga raina wa Niger, Victorien Adebayor.

Ni kikosi kilichokamilika na kuweza kushindana kama kingetaka kutwaa ubingwa. Pamoja na kuwa kiko imara ni kama kinachagua mechi za kucheza vizuri, hivyo kujikuta kikiachwa kwa pointi nyingi na Simba na Yanga.

Singida Black Stars inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 41, baada ya kucheza michezo 22.

Nafasi ambayo ipo ndani ya uwezo wao kwa sasa ni ya tatu na ya nne, ambayo itaifanya kucheza mechi za kimataifa msimu ujao, Kombe la Shirikisho Afrika.

Kama ikiendelea na tabia ya kuchagua mechi za kucheza vema na zingine kuzichukulia poa, inaweza kujikuta inashindwa kupata tiketi yoyote ya kuiwakilisha nchi na kuishia nafasi ya tano.

3# Tabora United

Timu hii ndiyo 'sapraizi' ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu. Baada ya kuponea kushuka daraja msimu uliopita kwenye 'play off', dhidi ya Biashara United, imekuja kivingine kabisa msimu huu. Ilianza kwa kusuasua, lakini ghafla, baada ya kuifunga Yanga mabao 3-0, Novemba 7, mwaka jana, iligeuka kuwa timu tishio na kuhofiwa na kila timu inayokwenda kukutana nayo.

Hata hivyo, kutokana na kufanya vibaya katika michezo kadha ya mzunguko wa kwanza imeifanya kutokuwa na nafasi ya kuwania ubingwa au kugusa nafasi ya pili, badala yake ina uwezo wa kutwaa nafasi ya tatu na ya nne na kuweka rekodi kucheza Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza.

Ina uwezo wa kuishusha timu moja chini kati ya Azam au Singida Black Stars. Imekusanya pointi  37 na ipo nafasi ya tano, tofauti na pointi nne tu na timu iliyo juu yake.