“Katika mwaka 2024/25 serikali itafanya kampeni maalum ya kutoa chanjo ya mifugo. Nami naunga mkono kwa sababu nimekubali kwamba serikali ibebe nusu ya gharama za chanjo, lakini nimefurahi kusikia kwa kuku chanjo ni bure maana najua ufugaji kuku ni mradi wa akinamama wengi,” anatamka Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Hiyo ameitoa katika kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Wakulima maarufu ‘Nanenane’ jijini Dodoma
Dhamira hiyo ya Rais Dk. Samia, inalenga kukabiliana na changamoto ya magonjwa ya wanyama yanayoikosesha nchi kukidhi matakwa ya kimataifa, kwa kukosa ithibati katika biashara ya mifugo na mazao yake kutoka Shirika la Afya ya Wanyama duniani (WOAH) na Shirika la biashara duniani (WTO).
Magonjwa yanayobainishwa yanatajwa kuweza kuwa na athari za kiuchumi, kibiashara na kwa afya za binadamu na serikali imeweka kipaumbele kukabiliana nayo ni:
Homa ya mapafu ya Nng’ombe (CBPP); homa ya mapafu ya mbuzi (CCPP); Ugonjwa wa miguu na midomo (FMD); mapele ngozi (LSD); Ugo kutupa mimba (Brucellosis); kimeta (Anthrax); sotoka ya mbuzi na Kondoo (PPR); ndigana kali (ECF); mdondo (NCD), marek; gumboro kichaa cha mbwa (Rabies); na Homa ya Bonde la Ufa (RVF).
Kukabiliana na changamoto ya magonjwa hayo ya Wanyama, sasa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imekuja na kampeni ya chanjo kitaifa ya miaka mitano (2024/2025 – 2028/2029) iikitarajiwa kugharimu shilingi bilioni 216.14.
“Kiasi hiki cha fedha kwa mwaka huu, kitatumika kununua chanjo za magonjwa ya Homa ya mapafu ya ng’ombe (CBPP) dozi 19,097,223, Sotoka ya mbuzi na kondoo (PPR) dozi 17,000,000 na magonjwa ya kideri, mafua (fowl coryza) na ndui kwa kuku dozi 40,000,000 na vitendea kazi,” anatamka Waziri Kijaji.
Anasema kwa mwaka uliopo, programu tajwa imelenga kuchanja dhidi ya magonjwa ya Homa ya Mapafu na Kideri/mdondo kwa kuku wa asili zitachanjwa kwa nchi nzima.
Aidha, anasema kwa ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo katika mikoa 14, ilikoathiriwa na ugonjwa huo, itachanja ambayo ni: Dodoma, Simiyu, Morogoro, Pwani, Mara, Manyara, Lindi, Mtwara,Tanga, Singida, Mwanza na Shinyanga.
NUSU GHARAMA
Anasema, ili kufanya programu ya uchanjaji kuwa endelevu, wafugaji watagharamia nusu gharama kwa kulipia kiasi cha shilingi. 500 kwa kila ng’ombe na Sh. 300 kwa kila mbuzi/kondoo.
“Kwa kuku chanjo hii itakuwa bure lengo likiwa ni kuwawezesha na kuwainua kiuchumi kina mama na vijana ambao ndio wafugaji wakubwa wa kuku wa asili. Aidha, anasema fedha zitakazo kusanywa katika programu hiyo ni Sh.Bilioni 13.18 zitakazosaidia kuendeleza kampeni ya chanjo awamu ya pili.
FAIDA YA KAMPENI
Waziri huyo anasema, kupitia programu hiyo, serikali inatarajia kupandisha idadi ya mifugo iliyochanjwa kutoka asilimia 22 ya sasa hadi 70 kwa magonjwa ya homa ya mapafu ya ng’ombe, sotoka ya mbuzi na kondoo, kideri, mafua na ndui kwa kuku.
Pia anasema, kuongezeka kwa uelewa, umuhimu na manufaa ya chanjo katika udhibiti wa magonjwa kutoka asilimia 30 ya kaya 4,202,744 za wafugaji hadi kufikia asilimia 70 na kutengeneza ajira 1,472 za muda mfupi kwa wataalamu walio nje ya mfumo rasmi wa ajira.
“Kuongezeka kwa biashara ya mifugo hai nje ya nchi kutoka mifugo 32,000 hadi 350,000 na kupata Sh.Bilioni 77.2 kwa mwaka; na kuongezeka mauzo ya nyama nje ya nchi kutoka tani 14,000 hadi 50,000 na kupata Sh.Bilioni 529.8 kwa mwaka.
“Nchi yetu imejaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa mifugo na kuwa nchi ya pili kwa wingi wa mifugo barani Afrika inakadiriwa kuwa na ng’ombe milioni 37.9, mbuzi milioni 27.6, kondoo milioni 9.1, kuku milioni 103.1 na nguruwe milioni 3.9.
“Hata hivyo, pamoja na utajiri huo, sekta ya mifugo inachangia kwenye pato la taifa asilimia 6.7. Mchango huu ni mdogo ukilinganisha na idadi ya mifugo iliyopo,” anasema Waziri.
Dk.Kijaji anaeleza kuwa Tanzania ikifanikiwa kuondoa vikwazo vya magonjwa kwa njia ya kuyadhibiti kwa kutumia chanjo itaweza kuuza tani 882,182.8 za nyama zenye thamani ya sh.Bilioni 9.3.
Pia, akataja mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka minne ya Rais Dk. Samia, kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 mpaka 2023/2024, serikali imejenga majosho ya kuogeshea mifugo yapatayo 548 na kukarabati majosho 1,014 kwa gharama ya Sh.bilioni 11,644.
Vilevile anasema, kiasi cha lita 147,907.75 za dawa ya kuogesha mifugo zenye thamani ya sh. bilioni 6.7 zilisambazwa na serikali.
“Juhudi hizi za ujenzi wa majosho, kusambaza dawa za kuogesha mifugo na kuhamasisha uogeshaji zimefanya kupungua kwa vifo vya mifugo vinavyosababishwa na magonjwa yasambazwayo na kupe na wadudu wengine, kupungua kutoka asilimia 72 ya vifo mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 45 ya vifo mwaka 2024,” anasema.
WADAU WASHIRIKI
Sasa Waziri Dk. Kijaji, anawaomba wakuu wa mikoa, wilaya, pia wakurugenzi wa halmashauri mijini na vijijini, vyama vya wafugaji na wadau wa maendeleo, kushiriki katika kampeni hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe, anasema utekelezaji wa chanjo hiyo unafanywa na watumishi wa ugani waliopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na wataalamu wa mifugo walio kwenye Sekta Binafsi, kwa kushirikiana na vyama vya wafugaji vilivyosajiliwa hapa nchini na wafugaji.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Taifa (CCWT), Mrida Mshota, anasema kazi ya chanjo, itawasaidia wafugaji kukabiliana na magonjwa ya mifugo, huku akimshukuru Rais Dk. Samia kwa kufanikisha hilo kufanyika kwa gharama nafuu, akitaka wizara kupatikana kipaumbele hasa kwa ugonjwa wa miguu na midomo (FMD).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED