Papa Francis atakumbukwa kutetea haki, upendo asiyejali wakosoaji

By Restuta James , Nipashe
Published at 05:38 PM Apr 24 2025
Papa Francis akikaribishwa Congo na Rais Felix Tshisekedi jijini Kinshasa Januari  31, 2023
Picha: Mtandao
Papa Francis akikaribishwa Congo na Rais Felix Tshisekedi jijini Kinshasa Januari 31, 2023

ILIKUWA Machi 13, 2013, Baraza la Makardinali lilipomchagua Kardinali Jorge Mario Bergoglio raia wa Argentina kuwa Papa, akichagua jina la Francisisko wa Asizi, kisha akaapishwa Machi 19, 2013.

Papa Francis (88), alisimikwa rasmi na kuwa Papa wa 266, akiitwa Papa Francis na kulitumikia Kanisa Katoliki kwa miaka 12. Aliaga dunia Jumatatu ya Pasaka wiki hii.

Papa ambaye mara kadhaa ametajwa kama mmoja wa watu wenye nguvu zaidi duniani, kutokana na ushawishi mkubwa wa kidiplomasia, kitamaduni na kiroho kwenye uga wa kimataifa atakumbukwa kwa juhudi hizi.

Mosi, kusaidia maskini, kuleta amani ya dunia, kutunza mazingira na ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa wote bila kujali dini, rangi au utaifa.

Padre Richard Mjigwa kutoka Vatican anamzungumzia Papa Francis kuwa aliamini maskini na wote waliowekwa pembezoni na jamii ni amana na utajiri wa kanisa na kwamba ndio walengwa wakuu wa habari njema ya wokovu.

“Hawa ni maskini wa hali na mali; wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na viungo vyake; wanaodhalilishwa na kunyanyaswa utu wao, heshima na haki zao za msingi. Ni wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa,” anasema Padre Mjingwa akikumbusha utume wa Papa Francis kutetea wahamiaji.

“Dunia inahitaji wajenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu, kwa kujikita katika majadiliano yanayofanywa katika ukweli na uwazi, kwa kuthamini, utu, heshima na haki za msingi za binadamu.

“ Waamini na wenye mapenzi mema, wawe ni wajenzi na vyombo vya amani duniani, manabii wa huruma na wasamaria wema, wanaothubutu kuwahudumia maskini kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu.” Alitaka Papa.

Ni katika muongo mmoja wa utume wa Papa Francis, imeanzishwa Siku ya Maskini Duniani, iliyoadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017, akisema siku hiyo ni kumbukumbu endelevu ya huruma ya Mungu.

Aliitaja siku hiyo kama fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya urafiki, umoja na udugu wa kibinadamu unaovunja kuta za utengano wa kimatabaka ya maskini na tajiri.

VITA TABIANCHI

Katika Waraka wa Kitume Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” anahimiza kutunza  nyumba ya wote ndiyo dunia”, anataka kulinda mazingira dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wote unaoiangamiza.

Baadhi ya mambo anayoyataja kuchafua dunia ni  migogoro ya kiikolojia na  vita.

Katika andiko hilo, Papa anasisitiza umuhimu wa kutunza ikolojia; haki, amani na udugu wa kibinadamu akiyataka mataifa kulinda na kutunza mazingira kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha maendeleo kwa wengi.

Akisimama kwenye diplomasia ya Vatican inajikita katika msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu; kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi.

Tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Papa Francis alisisitiza amani, kupambana na njaa na umaskini duniani, kwa kulinda na kutunza mazingira.

Anataja kuwa kuna mamilioni ya watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa fursa za ajira.

Katika Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti": unaomaanisha “Wote ni Ndugu”: Kuhusu udugu na urafiki wa kijamii” anachambua utamaduni wa udugu wa kibinadamu kama chombo cha ujenzi wa ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa.

Analenga zaidi kutafuta suluhu ya migogoro kwa njia ya mazungumzo akieleza kuwa vita vinasababisha maafa kwa binadamu na mali zao, vifo, vinaharibu mazingira pamoja na kufisha matumaini ya wengi.

Mara kadhaa anasisitiza kuwa majadiliano kwenye meza ya ukweli na uwazi ni njia ya kuvunja kuta za utengano kiakili na kwamba ni nguzo ya kufungua nafasi ya msamaha na kukoleza upatanisho baina ya mataifa na wanadamu.

Malengo ya "Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu kitaifa na kimataifa kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba jumuiya ya Kimataifa, vikiwamo vita; msisitizo ukiwekwa kwenye utawala bora unaozingatia sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kutekelezwa kwa manufaa ya watu wengi.

“Utawala bora unapaswa kuakisi matakwa ya jamii na si hisia za mtu binafsi,” anasisitiza.

Mara kadhaa, katika mahubiri yake, alitoa wito wa umoja katika jamii na kukosoa serikali ambazo zilishindwa kuwapa kipaumbele watu maskini zaidi katika jamii.

Aidha alifanya juhudi ya kuponya mpasuko kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Othodoksi la Mashariki, akifanya kazi na Waanglikana, Walutheri na Wamethodisti, kazi iliyoyaweka pamoja makanisa hayo.

Kadhalika, aliwashawishi marais wa Israeli na Palestina kuungana naye kuombea amani, akiwa mjumbe wa amani ambaye alikemea watu wanaouhusisha Uislamu na vurugu.

Akiwa raia wa Amerika Kusini anayezungumza Kihispania, alipatanisha Marekani na Cuba kwenye maelewano ya kihistoria. Ni vigumu kufikiria Papa wa Ulaya kuhusika katika jukumu muhimu kama hilo la kidiplomasia.

Katika juhudi za kusaka amani duniani, Papa alitembelea mataifa kadhaa na kufanya mazungumzo na viongozi wa dini nyingine wakiwamo Waislamu.

HAKUISAHAU AFRIKA

Papa  alizuru Sudan Kusini ambako aliwasihi viongozi wa nchi hiyo kumaliza migogoro, nchini Ukraine alitoa wito wa kukomesha vita.

Alifika  Kongo na nchi zinazotajwa kukabiliwa na vita na njaa, akihamasisha rasilimali zitumike kuwafikia masikini

Pia amezungumza na viongozi wa Marekani, Israel, Palestina na mataifa jirani kuhusu mzozo wa Gaza.

Jorge Mario Bergoglio, alizaliwa  Buenos Aires Argentina, Desemba 17, 1936, akiwa  mtoto wa kwanza kati ya watoto watano. 

Wazazi wake walikimbia nchi yao ya asili ya Italia ili kuepuka maovu ya ufashisti.

Aliwahi kuwa mlinzi wa klabu ya usiku na kufanya kazi ya usafi, kabla ya kuhitimu chuo akiwa mtaalamu wa kemia.