Polisi Rufiji na kampeni ya usalama kufikia bodaboda kata kwa kata

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 09:15 AM Feb 25 2025
Mkuu wa Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Miraji Mkojera na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Kata Mbwara, Faustina Ndunguru (kulia), wakitoa elimu kwa bodaboda.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Miraji Mkojera na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Kata Mbwara, Faustina Ndunguru (kulia), wakitoa elimu kwa bodaboda.

BODABODA inapenye kokote, ukiangalia pikipiki zinavyoendeshwa unaweza kudhani hakuna sheria zinazowaongoza. Wanachukulia kila jambo kwa urahisi kama vile barabara zote ni zao wenyewe.

Wanapita kokote mradi kuna mwanya bila kujali hatari inayowakabili, kuhatarisha maisha yao, abiria waliowabeba na watumia barabara wengine hasa vyombo vingine vya moto.” 

Ni wasi wasi unaoelezwa na Pili Kiiza, mwalimu wa shule moja ya msingi iliyo jirani na barabara jijini Dar es Salaam, anayesimama barabarani kusaidia wanafunzi kuvuka kila asubuhi na jioni, akiongeza kuwa pikipiki zimepewa majina mengi kama ‘mfalme wa barabara pia pepo wa mauti.’  

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji Pwani, limeona changamoto zinazosababishwa na ajali zinazohusisha bodaboda. Linaendesha kampeni ya kutoa elimu kwa madereva ili wafanye kazi bila kuhatarisha usalama wao na wengine barabarani, lakini watii sheria bila shuruti. 

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Rufiji, Protas Mutayoba, anafunga mafunzo ya utayari kwa wakaguzi wa polisi wa kata za mkoa huo ili washiriki kuwafunza bodaboda na kuelezea jinsi ambavyo ni lazima kulinda maisha ya watu na miundombinu kwa kutumia mbinu, sheria na vifaa.

Hatua hiyo inachukuliwa kutokana na ukweli kuwa ajali zinazotokana na bodaboda zinatisha. Mathalani, hivi karibuni bungeni linaarifiwa kuwa watu 1,113 wamepoteza kwenye ajali za bodaboda kuanzia mwaka 2022 hadi 2024.

Aidha, katika idadi hiyo ya waliofariki madereva walikuwa 759 wakati abiria waliofariki walikuwa 283 na wanaotembea walikuwa 71. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, ndiye anayetoa taarifa hiyo wakati anajibu swali la mbunge wa viti maalum, Fatma Toufiq, akitaka kujua idadi ya wananchi waliopoteza maisha kwa ajali za pikipiki kati ya mwaka 2022 na 2024. Licha ya bodaboda kuchukuliwa kama chanzo cha  ajira kwa vijana madhara yake ni makubwa kwa watumiaji na abiria, hivyo ni lazima kuwaelimisha na kuwapa mafunzo zaidi kila wakati.

“Mara ajali nyingi za bodaboda zinatokana na ukosefu wa elimu ya usalama barabarani kwa waendeshaji wa vyombo hivyo.” Anasema Kamanda wa  Mkoa wa Kipolisi wa Rufiji, Mutayoba.

Anasema wanawalenga ili wazingatie sheria za usalama barabarani, bila kujisababishia madhara  na kwa abiria na hata kwa waenda kwa miguu na miundombinu hasa barabara na vyombo vingine. 

Akifunga mafunzo hayo, kamanda huyo anakumbusha kuwa ni lazima kutumia kofia ngumu abiria na dereva wa boda na katika tukio hilo aligawa ‘helmeti’ kwa wakaguzi hao ili wakawape madereva wa bodaboda katika kata wanazosimamia ili wazitumie inavyotakiwa. 

Anasema kofia hizo zinatolewa kwa ushirikiano na wadau wa masuala ya usalama barabarani baada ya kuombwa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Faustina Ndunguru ambaye ni Mkaguzi wa Kata ya Mbwara mkoani humo. "Muwape kofia na mhakikishe mnatoa elimu kwa waendesha vyombo vya moto hasa bodaboda kutii sheria za usalama barabarani kwani Tanzania bila ajali inawezekana kila mmoja atimize wajibu wake," anasema Mutayoba. 

Anawaambia kuwa ni muhimu madereva wafundishwe kuhusu madhara ya ajali za barabarani, umuhimu wa kuvaa kofia ngumu ‘helmet’ kuwa na leseni za udereva na kuvaa vikoti vya kuakisi mwanga na kuacha  kukimbizana ovyo barabarani ili kunusuru maisha yao na watumia barabara wote. Kamanda huyo anasema elimu inayotolewa na Jeshi la Polisi inasaidia kuwajengea uwezo wa kutambua nafasi yao katika kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani. 

Anafafanua kuwa changamoto kubwa inayochangia ajali ni madereva hao kutozingatia sheria za usalama barabarani, kwa wengine kulewa au kujifunzia udereva vichochoroni na kuingia barabarani kubeba abiria. "Iwapo watazingatia elimu ya usalama barabarani inayotolewa na jeshi kwa kushirikiana na wadau wengine, anaamini ajali zinazotokana na uzembe haziwezi kutokea," anasema. 

Hadi Desemba mwaka 2024, madereva 200 kutoka kata ya Mbwara Rufiji, walipewa kofia na vikoti vinavyoakisi mwanga ili kusaidia kuwa salama zaidi wawapo barabarani, anasema Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Faustina Ndunguru.

“Kiuhalisia ni kwamba, uelewa mdogo wa sheria na kanuni za usalama barabarani bado ni changamoto kubwa kwa madereva wengi wa bodaboda, hivyo tumeamua kuwaelimisha," anasema Faustina.” Anasema katika kata yake kuna bodaboda 300, huku 200 kati yao wakiwa tayari wameshapata vifaa hivyo, na kwamba anaendelea na jitihada za kuhakikisha waliobakia nao wanapatiwa. 

"Tunawashukuru wadau  kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani kwa kutambua tatizo hili na kutupatia vifaa hivi ili kuwasaidia madereva wa bodaboda," anasema. Kamanda Faustina anasema wao wataendelea kuwajengea uwezo bodaboda ili watambue nafasi yao katika kufanya kazi ya udereva kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani waendelee kuwa salama. 

Katibu wa madereva wa bodaboda wa Kata ya Mbwara Fadhili Liato, anapongeza Jeshi la Polisi, wakiwamo wakaguzi wa kata  kwa jinsi wanavyojitahidi kuwajengea uwezo wa kutambua umuhimu wa kutii sheria za usalama barabarani na pia kushirikiana na jeshi hilo kutokomeza uhalifu na ukatili wa kijinsia. 

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Miraji Mkojera, anasema ajali za barabarani zina madhara yake, na kwamba ni muhimu madereva wa bobaboda kuvaa kofia ngumu. 

Anasema madereva wa bodaboda hawatakiwi kukimbizana barabarani ili kunusuru maisha yao. Wanatakiwa kuheshimu michoro ya barabarani, kukata bima za vyombo vyao na kutopakia mizigo kwa njia hatarishi. "Ajali za barabarani zinasababisha hasara kubwa kwa taifa, familia na jamii kwa ujumla. 

Hasara hizi ni pamoja na kupoteza wapendwa wetu ambao wengine tunawategemea, ulemavu wa kudumu na gharama kubwa za matibabu kwa waathirika wa ajali," anasema Mkojera. 

Mkojera anasema wakati polisi wanatoa elimu, ni vyema jamii kutambua kuwa inahusika kuhakikisha barabara zinakuwa salama kwa kutoa taarifa pale kuna vitendo hatarishi vinafanyika barabarani. 

Hadi kufikia Desemba 2024, kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba mwaka jana watu 453 walipoteza maisha.

Kwa mujibu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, vyanzo vya ajali ni pamoja na mwendo kasi wa dereva. Aidha, matumizi ya vilevi na madereva kuchukulia kuwa kunywa pombe na kufurahia maisha ni jambo la kawaida na wala si kosa yameangamiza wengi.

Jingine polisi wanalolitaja ni pamoja na kutumia simu wakati wa kuendesha. Wengine huweka foni masikioni na kufungulia muziki kwa sauti kubwa.

Kupuuza taa, alama na michoro ya barabarani na inakuwa mazoea siku hizi madereva kupuuza taa za barabarani na kukatiza bila kuzitilia maanani.

Kutofunga mkanda wa usalama na kutokuvaa kofia ngumu pia ni sababu.

Barabara pia ni chanzo kimojawapo cha ajali, zinaweza kuwa finyu, zilizobomoka. Pia za  vumbi ambazo huharibika kipindi cha mvua. Zipo zinazoteleza na kusababisha ajali.

Chombo chenyewe chaweza kuwa chanzo cha ajali mfano kufeli breki, steling kung’ooka, kupata pancha au tairi kupasuka.