MKUU wa Mkoa wa Shinyanga katika msimu wa kilimo uliopita 2023/2024, anatangaza kuwa ‘hakufanya vizuri kwenye zao la pamba,’ akitaja malengo iyakuwa kuvuna kilo milioni 30, lakini wakakomea kilo milioni 20.
Msimu wa kilimo 2024/2025, serikali mkoani humo imejiwekea malengo ya kuvuna kilo milioni 40 za zao la pamba kutoka kwa wakulima.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, katika kupambana anaamua kuingia shambani mwenyewe kunusuru zao la pamba, akinuia mavuno yanayofuata kuurudisha mkoa katika hadhi yake.
Dira anayopita nayo ni kurudisha hadhi yake kama ilivyokuwa miaka ya nyuma mkoani humo, nyenzo kuu ni kuhamasisha kilimo cha kisasa kinachomwinua mkulima kiuchumi.
Macha amekuwa akifanya ziara za kila mara, akiwatembelea wakulima wa pamba shambani, tangu ngazi ya maandalizi ya kilimo hadi sasa mavuno ya pamba yaliko.
Hapo kuna hatua za upuliziaji dawa na kuwahamasisha kuendelea kufuata kanuni bora za kilimo, ili wapate mavuno mengi.
Mkuu wa Mkoa anasema, zao la pamba mkoani humo lilishuka kasi ya kulimwa na wakulima, kutokana na mitazamo yao kuonekana ‘halilipi’ wakilalamikia bei ya pamba kuwa ndogo.
Anafafanua kuwa bei ya pamba siyo tatizo na kwamba shida ni wakulima wenyewe kupenda kulima kwa mazoea na kutofuata kanuni bora za kilimo, wakipenda kulima mashamba makubwa na kutumia gharama nyingi, mwisho wanaishia kupata mavuno kidogo.
“Nimeamua kufanya ziara ya kutembelea mashamba ya wakulima wa pamba kwa mkoa mzima, ili kuhamasisha kilimo cha kisasa.
“Msimu wa mwaka huu mkoa wa Shinyanga tumeweka malengo ya kwamba kila mkulima katika ekari moja anapaswa kuvuna kilo 1,200 au zaidi, na siyo kuishia kilo 250 mpaka 300,” anasema Macha.
Lingine analolitaja, kwamba mkulima anapopata mavuno kuanzia kilo 1,200 kwa ekari moja au zaidi, hawezi kulalamikia bei ya pamba, kwa sababu atapa pesa nyingi inayomtoa kwenye umaskini.
HISTORIA MKOA
Macha, anasema historia ya mkoa wa Shinyanga, wapo wakulima miaka ya nyuma waliwahi kupata wastani wa kilo 1,800 hadi 2,000 kwa ekari moja.
Hiyo inatajwa kufanikisha uhakika wa makisio ambayo wamemwekea mkulima, kuvuna kilo 1,200 kwa kila ekari, kuwa jambo linalowezekana.
“Kipindi ninaapishwa na Rais DK. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, moja ya maagizo aliniambia nije kusimamia zao la pamba na kurejesha heshima yake kama zao kuu la ukuzaji uchumi kwa wananchi.
“Ndiyo maana nimeamua kuingia shambani kuhamasisha kwa vitendo kilimo cha kisasa,” anasema Macha.
Kwa mujibu wa taarifa za Bodi ya Pamba Tanzania, asilimia 40 ya Watanzania hunufaika na zao hilo katika mnyororo wa thamani, kuanzia uzalishaji, ununuzi, uchambuaji, usafirishaji, mauzo nje ya nchi na uzalishaji wa nguo hapa nchini.
SAUTI YA WAKULIMA
Mkulima wa pamba, Andrew Maganga, kutoka kijiji cha Sayu wilayani Shinyanga, anasema baada ya kupata elimu ya kilimo bora cha zao la pamba, amekuwa akilima kisasa, akpanda mbegu za pamba sentimita 60 kwa 30, ikimpa mavuno mengi.
Anasema, katika msimu wa mwaka jana 2023/2024, alilima pamba ekali moja na robo zilizozalisha jumla ya kilo 2,760, na akatunukiwa kuwa mshindi wa pili kitaifa wa uzalishaji pamba, akazawadiwa na serikali, fedha shilingi milioni tano.
Mkulima mwingine George Bulugu, anasema mwaka jana amelima kisasa ekari mbili za pamba, ikampatia kilo 1,800, huku matarajio yake mwaka huu, ni kuvuna zaidi, akitaja sababu ni kuwapo mvua za wastani.
Mkulima Shimba Sprian, anasema elimu ya kilimo cha kisasa ni muhimu kwa wananchi na anampongeza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, kuamua kulivalia njuga zao hilo, ikiwamo kwa kuwatembelea wakulima shambani tangu mwanzo wa maandalizi ya kilimo hadi sasa.
WADAU KILIMO
Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Shinyanga, Ansila Karani, anasema katika msimu wa kilimo wa zao la pamba katika mwaka wa kilimo ulioko, ambayo wamejiwekea ni kulimwa ekari za pamba 67,173 na kuvunwa kilo 40,63,200.
Anasema, matarajio hayo ya kuvunwa kilo milioni 40 za pamba sasa, anayataja yanaweza kufikiwa au kuvuka lengo, kutokana na wakulima kuhamasika kufuata kanuni za kilimo bora, na mashamba mengi yanaridhisha pamba yake.
Anasema msimu wa kilimo 2023/2024 hawakufanya vizuri kwenye zao la pamba, ambapo malengo ilikuwa ni kuvuna kilo milioni 30, lakini hawakuweza kuzifikisha kutokana na baadhi ya wakulima kupuuza kilimo cha kisasa na hawakuvuka kilo milioni 20.
Waziri wa kilimo, Hussen Bashe, alipokuwa akizindua Kampeni ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mkoani Shinyanga, mnamo Novemba 20,2024, akasema serikali imedhamiria kuiinua zao la pamba na kumyanyua mkulima kiuchumi, ikiwapatia pembejeo bure za kilimo, zikiwamo mbegu na dawa.
Akaahidi katika msimu wa kilimo 2024/2025, wataiimarisha zaidi bei ya pamba na itakuwa ikibandikwa kwa kila AMCOS kwenye mbao za matangazo.
Pia, inaelezwa kuwa risiti za mauzo mkulima atakuwa akipewa saa 9.00 mchana, ili apate malipo halali kulingana na bei husika, sababu bei ya pamba itakuwa ikibadilika kila wakati.
Bei elekezi ya ununuzi wa pamba katika msimu uliopita 2023/2024, ilikuwa shilingi.1,150 kwa kilo moja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED