Sababu Salah kukataa mamilioni ya Waarabu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:22 PM Apr 22 2025
Mo Salah
Picha: Mtandao
Mo Salah

MOHAMED Salah anabakia Liverpool na hivyo kuhitimisha moja ya habari kuu za msimu huu. Hata hivyo, nyakati fulani ilionekana kuwa na shaka.

 Saudi Arabia alitengewa kiasi cha pauni milioni 500 na mshambuliaji huyo wa Timu ya Taifa ya Misri akaamua kuikataa na kuamua kusaini mkataba mpya utakaodumu hadi atakapofikisha miaka 34.

Mwanahabari mkuu wa soka wa BBC Sport, Sami Mokbel anaripoti...

Mafanikio ya makubaliano yalikuja Machi, mwishoni. Salah alipofichua kuhusu hatima yake Novemba, mwaka jana kwa kusema 'amejitenga zaidi kuliko kuwa ndani'.

Lakini pia Mmisri huyo alitaka kubakia Liverpool. Misimamo hiyo miwili haikuwa lazima iwe ya kipekee.

Imekuwa ni dhamira ya Salah kuongeza muda wake wa kukaa Anfield kwa miaka nane - na habari za sasa za mkataba wake mpya wa miaka miwili zitamfanya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 kuhudumu katika klabu hiyo kwa mwongo mmoja, endapo ataondoka muda wa makubaliano hayo utakapokamilika.

Lakini masharti - kwa Salah na Liverpool ilibidi yawe sawa.

Vyanzo vilivyo karibu na hali hiyo vilidokeza mafanikio katika mazungumzo kati ya Salah, mwakilishi wake, Ramy Abbas Issa, na Mkurugenzi wa Michezo wa Liverpool, Richard Hughes, yalifikiwa Machi, mwishoni na taratibu za mpango huo kuhitimishwa mapema wiki hii.

Hakika, katika mahojiano na BBC Sport, beki wa kushoto, Andy Robertson, alifichua alijua tu kuhusu mkataba mpya wa Salah Alhamisi ya wiki iliyopita.

Salah hakupunguza mshahara ili kubakia Liverpool - na atalipwa pauni 400,000 kwa wiki. Mkataba wa miaka miwili unampa kiwango cha usalama kwa wachezaji wa umri wake. 

'KESI MAALUMU'

Liverpool wamesukuma mashua nje, lakini hawajafanya hivyo kwa matakwa. Salah ni kesi maalum.

Kutafuta nafasi ya mshambuliaji wao mahiri, ambaye tayari amechangia mabao 54 msimu huu, ingekuwa ngumu sana na haswa, kazi ya gharama kubwa.

Kumtambua mbadala wa Salah ingekuwa ngumu vya kutosha, lakini kutafuta aina ya fedha ili kumaliza mpango kama huo kungeleta ugumu wa hali ya juu.

Kama Trent Alexander-Arnold, angeuzwa kwenda Real Madrid ingewapa Liverpool fursa kubwa ya kifedha katika juhudi zao za kukusanya fedha kuwabakisha Salah na Virgil van Dijk, lakini Mwingereza huyo anaondoka kama mchezaji huru.

Hata hivyo, ingawa fedha huwa ni jambo la msingi linapokuja suala la mazungumzo ya kimkataba, haikuwa hivyo kwa Salah.

FEDHA SIO SULUHISHO

Iwapo fedha ndiyo ilikuwa uamuzi wa Salah, angeondoka Liverpool na kwenda Ligi Kuu ya Saudia, ambao hadi wiki iliyopita, bado waliamini wangeweza kumvutia Mashariki ya Kati.

Ushawishi wa kifedha wa kuhamia Saudi Arabia ulikuwa wazi.

Hakika, vyanzo vimeiambia BBC Sport, Salah alikuwa tayari kupata angalau pauni milioni 500 nchini Saudia.

Ilisemekana chaguo la kuchunguza hatua ya Saudia liliibuliwa kwa mara ya kwanza na Salah tangu Februari, mwaka jana na mlango huo huenda ukabaki wazi katika siku zijazo.

Lakini, hivi sasa, fowadi huyo ameweka tamaa ya fedha nyuma ya mipango yake.

Salah ni mchezaji anayeongoza mchezo wake - wale walio karibu na mshambuliaji huyo wanaamini ana angalau miaka mitatu kwenye kiwango cha juu zaidi cha kuendelea kucheza.

Ushahidi unapendekeza hivyo. Mwili wake ni bora na utimamu wake upo sawa.

Salah anaamini bado ana mengi ya kutimiza katika soka la Ulaya, akianza, bila shaka, kwa kushinda taji la 20 la ligi kwa Liverpool msimu huu.

Ana matarajio ya kushinda Ballon d'Or pia, na alikuwa nafasi ya tano mwaka 2019 na 2022.

Salah pia anataka kushinda tena Ligi ya Mabingwa Ulaya, na kuhakikisha Liverpool inabakia katika kilele cha soka la England.

Jambo la kufurahisha, inasemekana sababu nyingine muhimu katika uamuzi wake wa kusaini tena ilikuwa nia ya kushindana miongoni mwa wachezaji wakubwa ili kusaidia kujiandaa kwa ajili ya kampeni zijazo za Misri za Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa ya Afrika.

Ni changamoto ya kimichezo ambayo imesababisha uamuzi wake kwa Salah, ingawa ukweli ni mkewe, Magi na binti zake wawili, Makka na Kayan, wanafurahia zaidi maisha ya England kuliko kwenda Arabuni.