MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, amesema hatakaa kimya wakati wakulima wa tumbaku mkoani Tabora wamedhulumiwa fedha zao na vyama vya ushirika, akiagiza kupelekewa taarifa kamili za madai hayo ili aifikishe serikalini.
Akiwa ziarani mkoani Tabora kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM, Wasira anapokea malalamiko kutoka kwa wakulima mbalimbali wakivitupia lawama vyama vya ushirika kushindwa kuwapatia haki zao.
Akiwasilisha malalamiko hayo Brison Nyamwenda, mwanachama wa Chama cha Ushirika cha Msingiti Sanga, anasema msimu wa 2022-23 chama hicho kilizalisha zaidi ya Shilingi bilioni moja, lakini viongozi walijinufaisha wenyewe, na wakulima hawakulipwa fedha zao.
Anasema hatua mbalimbali zilichukuliwa na serikali kutowa baadhi ya maagizo lakini utekelezaji wake umekwama hadi sasa.
Anasema kuna mkulima mmoja miongoni mwa waliodhulumiwa amefikisha kesi yake katika mahakama ya wilaya kuwasilisha madai ya kudhulumiwa na kesi ilihukumiwa na kwa kumpa ushindi mlalamikaji ambako mahakama ilitoa notisi ya kuuzwa maghala ya chama hicho.
"Wakulima wanaodai ni takribani 232 lakini haki imetolewa kwa mmoja, tunaomba kusaidiwa kwasababu hili linatuhusu sote. Ifahamike kuwa hiki ni kipindi cha masoko lakini wakulima wameshindwa namna ya kukushanya tumbaku zao kwasababu maghala tayari yameshafungwa," anasema Nyamwenda.
Sadiki Ramadhani, ni mkulima mwingine anayezungumzia sakata hilo akisema kero yake kubwa iko kwenye fedha ya ruzuku kwa wakulima wa tumbaku ambayo ilitolewa tangu mwaka jana, lakini hadi sasa haijawafikia licha ya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kuwaahidi fedha hiyo itatoka lakini hadi leo ni kimya.
Julius Patrick, mkazi wa Urambo alikumbusha kuwa ni zaidi ya miaka minne kuna kampuni ya mazao ambazo ziliingia nchini na kubeba mazao ya wakulima lakini bila kulipa na sasa vyama vimeyumba kwasababu kampuni hizo ziliondoka na fedha zao.
Kadhalika kampuni hizo zimeondoka na nyaraka muhimu za madai ya vyama hivyo, kumuomba Mwenyekiti wa CCM wasaidiwe katika kupata haki yao, anaungwa mkono na Paschal Emmanuel, kutoka Chama cha Msingi cha Ibelamilungi, anasema msimu wa 2023-24 waliiuzia kampuni ya Moldisel takribani kilo 676,152 za tumbaku lakini hawajalipwa.
Asema mazao yao yana thamani ya zaidi ya Dola milioni 1.7 na kwamba hadi sasa kampuni hiyo imekilipa chama hicho dola 119,000 sawa na Shilingi 319,541,835.69.
"Madai ambayo wakulima wanaidai kampuni hiyo ni zaidi ya Dola 700,000, sawa na Shilingi 1,879,657,857, tumewasilisha changamoto hii tunaomba wakulima tuangaliwe tulipwe tuna hali mbaya na kipindi hiki ni kibaya zaidi tunaelekea kwenye masoko na tumbaku pekee tunaitegemea kutuingizia kipato," anasema Emmanuel.
ANASISITIZA WASIRA
Kutokana na malalamiko hayo Wasira anamwagiza Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Tabora kuorodhesha malalamiko yote ya wakulima ambao hawajalipwa na yafikishwe kwake ili yaende serikalini kwa maamuzi zaidi.
"Msingi mkubwa wa ushirika ni ushirikiano wa watu kwa ajili ya kujibu matatizo yao, na kusaidia wanachama wetu, lakini udhaifu mkubwa wa vyama vya ushirika ulitokana na ubinafsi, ndani ya vyama hivyo tukisema wewe ndiye kiongozi wetu ni lazima upunguze ubinafsi ili tupate faida.
"Ushauri wangu kwa vyama vya ushirika mjitahidi kuwa waaminifu kwasababu kinachoua vyama hivi ni kukosekana kwa uaminifu na uadilifu, kulinda mali za ushirika ni jambo la msingi kwasababu kama hamzilindi ushirika haupo, kinachofanya mshirikiane ni mapato yenu yanayotokana na kushirikiana, sasa kama hamyalindi ni kama mnajiandaa kusambaa," anasema Wasira.
Wasira anashauri viongozi kujaribu kuimarisha vyama vya ushirika kwa kuwa waaminifu kwa dhati, pamoja na kuwasomesha watu katika vyuo vya ushirika ili wale wanaofanya mahesabu kwenye vyama hivyo wazifanye kwa ufanisi kuwanufaisha wanachama wake.
Pia, anashauri kuwa benki ya ushirika inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni waweke masharti nafuu ili iwasaidie wakulima kupata mikopo kwa urahisi, kwasababu kama itakiwa sawa na benki za biashara utofauti wake na zingine utakuwa hakuna.
"Wakulima dunia nzima hawakopesheki hasa wadogo, mimi napenda ushirika lakini nataka kuona unafanikiwa si kufa, lakini msisitizo wangu kulingana na hayo mliyoyasema, mjaribu kuimarisha uaminifu ndani ya ushirika ili tuwe na mfumo shindani unaoweza kusaidia kukuza na kuendeleza ustawi wa wanachama na wananchi kwa ujumla," anasisitiza Wasira.
ATANGAZA HATUA
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Tabora, Venance Msafiri, anaahidi kuyafanyia kazi huku akisema Tabora wameshaanza kusomesha watendaji wa vyama hivyo, na wajumbe wa bodi akieleza kuwa hatua hizo ni katika kutatua changamoto zilizoko.
Anaeleza kuwa katika mpango huo tayari wamefikia watendaji 400, wajumbe wa bodi 1,500 na wanachama 4,000 akieleza kuwa mchakato huo utakuwa endelevu kuwapa elimu kila mwaka.
“Tunafahamu jinsi gani ulivyokuwa unapambania huu ushirika, lakini suala la pembejeo miaka ya nyuma zilikuwa zinasambazwa na kampuni za tumbaku na wakati Wasira ulipokuwa Waziri wa Kilimo ulifanya maamuzi magumu na kuelekeza zisambazwe na vyama vya ushirika.
“Katika suala la ruzuku tayari ziko bilioni 13 na kuna timu zinakamilisha kuhakiki malipo na ndani ya siku saba mchakato huo utakuwa umekamilika na wakulima wataanza wa kulipwa. Wapo zaidi ya 57,000 watakaonufaika na pembejeo,” anasema Msafiri.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED