SIKU 10 ZA MOTO CCM KUSINI; Yahamasisha uchaguzi wa amani

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 05:48 PM Apr 24 2025
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla
Picha: Maulid Mmbaga
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla

CHAMA Cha Mapinduzi kimewatoa hofu Watanzania kuwa watafanya uchaguzi mkuu wakiwa salama na kuumaliza bila kutetereka.

Ni ahadi ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla (pichani), akiwa mkoani Lindi, akisema: “Tutahakikisha amani na utulivu wakati na baada ya uchaguzi kwa kuwa tunafahamu hakuna nchi nyingine, tutatofautiana kimtazamo, kisiasa, kiitikadi, lakini Tanzania itabaki moja,” anasema.

Makalla akiwa katika ziara ya mikoa ya kusini hivi karibuni iliyoanza mapema mwezi huu (Aprili 10 hadi  18) akizitembelea wilaya za mikoa ya Lindi na Mtwara, amehamasisha kulinda amani na kushiriki uchaguzi mkuu.

Anasisitiza kuwa, amani iliyoko ni muhimu na kuwataka Watanzania wasiruhusu ichezewe  na kuwataka wawakatae wanaohubiri uvunjifu wa amani.

FURSA ZA KIUCHUMI 

Katika ziara hiyo, Makalla  anawaeleza wananchi nia ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuifungua mikoa ya  kusini kiuchumi kwa ujenzi wa barabara na kuboresha Bandari ya Mtwara.

Anaitolea mfano barabara ya kiuchumi yenye urefu wa kilometa 210 inayoendelea kujengwa kutoka Mtwara-Nanyamba-Newala hadi Masasi, ikigharimu Sh. bilioni 234, ambayo Rais Samia aliiwekea jiwe la msingi.

“Rais Samia amenituma, akaniambia ‘Mwenezi ukienda huko ukague na hiyo barabara ya kilometa 210, kilometa 50 ziko tayari angalia kama ujenzi unaendelea’.

“Nimethibitisha, nimemkuta mkandarasi, maandalizi yanafanyika, vipande viwili kilometa 100 amepewa mkandarasi mmoja, kilometa 60 kachukua  mwingine zote 210 mpaka Masasi zinajengwa,” anasema.

Kuhusu Bandari ya Mtwara, Makalla anawaambia wananchi kuwa kwa kuanzia serikali itatoa Sh. bilioni 157 kuiboresha na kuipanua.

Anaongeza kuwa barabara hiyo itakapokamilika itaunganisha  Mchuchuma, Mbamba Bay na Bandari ya Mtwara na maeneo mengine na kurahisisha usafirishaji wa mazao hasa korosho. 

Amewahakikishia fidia wananchi  waliopisha barabara hiyo akisema  tayari Sh. milioni 428 zimeshafika kwa ajili ya malipo hayo.

MAAGIZO

Barabara nyingine ambayo aliizungumzia na kutoa maagizo kwa Wizara ya Ujenzi ni ya Nangurukuru-Liwale yenye urefu wa kilometa 237 ambayo yote ni ya vumbi.

Baada ya kupita katika barabara hiyo na kujionea adha wananchi wanayoipata, Makalla akiwa kwenye mkutano wa hadhara wilayani Liwale, alimpigia simu Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, na kumweka mbashara na kumtaka aende kutatua kero hiyo.

“Ninakuomba mambo mawili kwa kuwa upo Lindi usipite barabara nyingine pita Nangurukuru mpaka hapa Liwale,” anaelekeza.

Baada ya maelekezo hayo, Waziri Ulega anawaahidi  wananchi kufika huko na kwamba barabara hiyo itajengwa.

Changamoto nyingine ambayo Makalla aliambiwa ni kuhusu wanyamapori, ambapo pia, baada ya kumpigia simu Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana, lakini haikupokelewa simu.

Akawaeleza wananchi kuwa awali aliwasiliana na waziri huyo na kumweleza changamoto hiyo ambayo naye ameahidi kufika hapo ili aweze kuona namna ya kutatua.

Changamoto nyingine iliyoibuliwa ni ya umeme, ambayo Makalla alizungumza na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, ili kuona namna  umeme utakavyotoka Dar es Salaam kupitia Rufiji hadi Somanga ili utumike kwenye  shughuli za uzalishaji kwenye migodi, badala ya kutegemea unatoka Ruvuma kupitia Mtwara kwenye gridi ya taifa.

Akizungumzia pia, changamoto ya kukatika mawasiliano ya daraja la Somanga-Mtama, lililoko Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, anawaahidi wananchi wa mikoa ya kusini kuwa serikali inatafuta ufumbuzi wa kudumu.

“Niwatoe wasiwasi Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi na Rais Samia, amemwelekeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kutia timu  ili kuhakikisha mawasiliano ya mikoa ya kusini yanarejea,” anasema.

UBADHIRIFU

Katika ziara hiyo, Makalla amekerwa na wabadhirifu katika vyama vya ushirika aliowafananisha na ‘mchwa’ huku akitaka washughulikiwe.

 “Nimefurahi kupokea taarifa kutoka kwa Ofisa Ushirika Mkoa, ambapo jitihada za serikali ni kusaidia vyama vya ushirika na wakulima katika kupata bei katika kuongeza pembejeo na kusababisha maisha ya watu kubadilika siku hadi siku.

“Nyie ni mashahidi wakati wa kangomba bei ya korosho ilikuwa shilingi ngapi na sasa ni shilingi ngapi? Nimewaeleza Kilwa kuwa katika wale viongozi wanaopotosha wananchi hakuna hata mwenye shamba, hawajui kulima na hawajui mazao haya,” anasema.

Makalla anawaambia wananchi waendelee kushirikiana na serikali, kwa sababu Rais Samia ameingia katika rekodi ya kubadilisha maisha ya wakulima, kuongeza ruzuku ya pembejeo ya mbegu na mbolea.

“CCM kwenye ilani tumeongeza mipango yetu kuboresha ushirika, hao wengine hawana dhamana wala wajibu, wasikilizeni viongozi wenu.  Tunatambua wapo mchwa na watu wabadhirifu kwenye vyama vya ushirika, hao ndio watu wa kushughulika nao,” anasema.

Makalla amewaeleza wananchi umuhimu wa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani, akisisitiza kuwa umesaidia bei ya zao hilo kupanda hadi Sh. 4,000 na kukuza uchumi, ikilinganishwa na huko nyuma.

AWAJIBU UPINZANI 

Akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Masasi Mjini, Makalla anasema: “Juzi nilimsikia John Heche, Makamu Mwenyekiti CHADEMA, akizungumzia makaa ya mawe yanabebwa malori kwa malori kwenda nje huku vijana wakibaki na mashimo,  anasema tumeshindwa kuendesha bandari.”

Akijibu hoja hiyo, Makalla anasema: “Kuuza makaa ya mawe nje si haramu, ni kuongeza mapato ya nchi. Lakini si kila gari unalokutana nalo linayapeleka nje, viwanda vya saruji vinahitaji makaa ya mawe yanayotoka kusini, makaa ya mawe ni fursa kwa viwanda vya Tanzania na fursa kiuchumi kwa kupeleka nje ya nchi pia.”

BANDARI DAR

Makalla pia, anazungumzia maboresho makubwa yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam kuwa  kabla ya  kampuni ya DP World inayoshusha na kupakia makontena kwenye bandari ya Dar es Salaam  uondoaji wa makasha hayo ulichukua siku 40, lakini  sasa haizidi siku tatu.

“Makontena kwa mwaka mmoja yameongezeka hadi 1,000,000  bandari yetu inakuwa ya mfano Afrika Mashariki, mapato ya serikali yameongezeka, biashara imeongezeka, uagizaji umeongezeka na gharama pale za usafirishaji kontena zimeanza kupungua,” amesema.

AONYA KUJIPITISHA 

Katika hatua nyingine, Makalla amesema kupitia utaratibu mpya wa mabadiliko ya katiba ya CCM na kanuni za uchaguzi, wanakwenda kudhibiti wanaojipitisha majimboni kuharibu hali ya hewa wakiwamo wanaojiona wana mfuko mkubwa wa fedha.

Akiwa wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, katika mkutano wa ndani, kiongozi huyo alisema kwamba, mabadiliko hayo yamefanyika kwa njia njema.