Songwe; Mapinduzi utafiti udongo, kuinua kilimo kahawa chenye tija

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:10 PM May 01 2025
Kahawa
Picha: Mtandao
Kahawa

KWA anayeufahamu mkoa wa Songwe, wasifu wake kiuchumi umezama katika kilimo.

Kama ilivyo kwa majirani zao mkoa wa Mbeya, wamezama katika kilimo, ilhali hata katika ufugaji nako ‘hawajambo.’ 

Ni mkoa ulioko katika ngazi tegemezi kitaifa katika kuzalisha baadhi ya mazao, hapo ikitajwa mojawapo ni kahawa ambayo sasa iko nchini kwa karne moja na nusu.

Hili ndilo linalowafanya wakulima wake nao leo kupaza sauti katika jambo la kifundi shambani, wakiwataka wasomi wa kilimo na fani zinazofanana nazo kufanya utafiti katika afya ya udongo, ili kuongeza tija ya zao husika - kahawa.

Ni rai inayoelekezwa mahsusi kwa Taasisi ya Utafiti wa Mbegu Tanzania (TACRI) kuwawezesha wataalamu kufanya tafiti za afya ya udongo ili kuongeza tija ya zao hilo.

Maandalizi ya mbegu ya kahawa katika ngazi tofauti
Mkoa wa Songwe kupitia wilaya yake Mbozi, ndio leo inashika nafasi ya pili kitaifa kwa uzalishaji wa zao la kahawa, ingawaje inatajwa kiwango chake katika siku za hivi karibuni, uzalishaji unatajwa kushuka, huku wakulima wakiwa na uhaba wa mbegu.

Dismas Pangalas, ni Meneja wa Kanda wa TACRI, ambaye licha ya kukiri changamoto ya uhaba wa mbegu, lakini anaeleza mikakati waliojiweka kukabiliana na uhaba huo.

Anasema wanazalisha mbegu nyingi, lakini bado haitoshelezi mahitaji ya wakulima.

Meneja Pangalas, anaeleza kwamba mwaka jana walizalisha miche milioni nane kwa kanda nzima, huku wilaya ya Mbozi pekee walizalisha miche milioni 3.36 (asilimia 42) lakini hata hivyo haikutosha.

Maandalizi ya mbegu ya kahawa katika ngazi tofauti
Anasema kutokana na hilo, wamewaunganisha wakulima wakubwa na kati, wakiwajengea uwezo na elimu, kisha kuwawapatia udongo na mbegu wakizalisha miche itakayogawiwa kwa wakulima wadogo, kupitia vyama vyao.

Kwa wilaya ya Mbozi pekee anasema kuna vyama 18 vya ushirika, huku ujumla wake kikanda vipo 26. Hapo kunatajwa hadi sasa kumeshafanywa tafiti aina 19 za mbegu.

Kwa mujibu wa meneja huyo, hadi sasa wameshapanda mbegu aina chotara ziitwazo ‘Compact’ inayohimili magonjwa.

Pangalas anasema, katika miaka ya hivi karibuni uzalishaji wa kahawa wilayani Mbozi ulishuka, kutokana na kuyumba hali ya hewa kitaifa, ikiwamo kutonyesha kwa mpangilio, kwani kahawa inahitaji kupata mvua kwa miezi sita.

Anataja tatizo lingine ni kupitiliza kwa joto linalopaswa kuwapo mwaka 2023, /2024. Ni kipindi kilikuwa na nyuzi joto 30 hadi 33. Ni kiwango kisichowiana, maana ilitakiwa kuwa chini ya hapo, hata kusababisha kuwapo mbadala kimkakati wa kuletwa kilimo cha umwagiliaji.

‘’Serikali inatambua, hivyo mpango uliopo ni kujenga mabwawa kwenye mashamba ili kahawa iwe inamwagiliwa kukabiliana na mtawanyo mbaya wa mvua,” anafafanua Pangalas, kwa lugha ya kitaalamu.

HISTORIA YA KAHAWA 

Meneja Pangalas anasimulia historia kuwa zao la kahawa liliingizwa nchini kwa mara ya kwanza mwaka 1880 kupitia Bandari ya Kilwa, waingizaji wakiwa Wamissionari. Baada ya kupandwa, ikaungua, lakini ikapandwa tena wilayani Moshi, ‘ikakubali’.

Anaeleza historia hiyo, kwamba wilayani Mbozi, kahawa iliingizwa mwaka 1910 hadi 1915 ikipandwa katika kijiji cha Mbozi (Mbozi Mission).

Inafafanuliwa kwamba aliyeuleta nchini kutoka barani Ulaya, aliitwa Jesuit Benchman. Baada ya hapo, bidhaa hiyo ikaendelea kusambaa katika maeneo mbalimbali na masoko yake yakiwa nchi kama Japan na kwingineko.

Anasema katika eneo la utafiti wa mbegu, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambako leo hii kuna makao makuu wilayani Mbozi mkoani Songwe.

Hapo kunatajwa leo kijijini Mbimba kwenye jumla ya hekta 132 za kahawa, kumewekwa lengo la kuzalisha mbegu kati ya milioni nane hadi 10 kwa mwaka.

Anasema walitoa elimu kwa wakulima kupanda mazao mseto (mazao mchanganyiko) katika kil aekari wachanganye migomba, kahawa, parachichi, mboga na miti ya kivuli.

WAKULIMA WAWEZESHAJI VITALU 

Benard Haonga, ni mkazi wa kijiji cha Mbozi (Mbozi Mission) anasema yeye ni mkulima wa Kahawa ambaye analima kilimo mseto kwa kuchanganya na parachichi pamoja na migomba huku akijikita zaidi katika uzalishaji wa miche ya kahawa na miti ya asili.

Anasema kutokana na zao hilo kushuka wilayani Mbozi, wameingia mkataba na Bodi ya Kahawa nchini iwawezeshe, vifaa ikiwamo udongo, mbegu na uzio.

Haonga anataja kuwa mwaka jana alifanikiwa kuzalisha miche 300,000 na mwaka huu amezalisha miche 3,500,000.

Mbali na kujihusisha na kahawa, pia anasema anajishughulisha na upandaji miche ya miti ya asili kwa ajili ya kupanda maeneo yenye vyanzo vya maji, ili kulinda uoto wa asili na kulinda mazingira akishirikiana na maofisa wa TSF.

Anataja changamoto iliyopo kwao ni ukosefu wa elimu ya afya ya udongo, kwani wakulima wengi wanapanda kwenye udongo wenye wadudu, hata inawafanya kupata hasara kwa mazao yao kutochipua na hata ikichipua, inaishia kukauka na kushambuliwa na wadudu.

Kwa mujibu wa Haonga, miche hiyo inagawiwa kwa wakulima kupitia vyama vyao, lengo likiwa ni kukabiliana na uhaba huo wa mbegu.

Anaeleza taasisi ya utafiti TACRI, inapozalisha mbegu zake, hazitoshelezi, hivyo wameweka utaratibu wa kuwezesha wakulima wa kati kuzalisha mbegu, ili kuondoa uhaba uliopo.

WAKULIMA WAFUNGUKA 

Chriss Nzunda, ni mkulima kutoka kijiji cha Masangula, anasema ameingia mkataba na TACRI, hata akafanikiwa kuzalisha miche 100,000, huku akiajiri vijana wanaowezesha kufanya kazi hiyo.

Anasema binafsi ana shamba darasa la mazao mseto, yaani kahawa, migomba na parachichi yaliyopandwa katika shamba moja na wakulima wadogo wanaofika kujifunza namna ya upandaji ulivyo.

Vilevile Tinson Nzunda, mkulima kutoka kijiji cha Masangula, ambaye naye ameingia mkataba na taasisi hiyo yeye amezalisha miche 300.000 ambayo itagawiwa kwa wakulima ili kupunguza changamoto ya uhaba wa mbegu, kutokana na kuwapo mwitikio mkubwa wa wakulima wanaotaka kupanda kahawa.

Mkulima Aloyce Mdalavuma, ambaye ni Diwani wa Kata ya Bara, anasema amepanda miche 100,000 ya mbegu chotara ya aina ya ’Compac’ inayohimili magonjwa, huku akiishukuru Bodi ya Kahawa nchini kwa kuwa karibu nao.

Katika eneo hilo la Nyanda za Juu Kusini, wilaya zingine zinazozalisha kahawa zinajumuisha Rungwe na Mbinga, uzalishaji ukiwa katika rekodi ya ufanisi.

•   •  Mwandishi anapatikana kwa mawasiliano: yassin.ibrahimu@yahoo.com au simu: + 255 718382817